*Rais Magufuli awapa maagizo 12 wakuu wa mikoa
*Awatangazia kiama vijana wanaocheza pool table
Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amewaapisha wakuu wa mikoa wapya 26, huku akiwapa maagizo 12 muhimu ikiwamo kuwaweka ndani watendaji wanaonyanyasa wananchi.
Pamoja na hayo, amesema kwamba baada ya kuapishwa kwa Kamishna mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mkurugenzi wa Takukuru, anaamini watafanya kazi na mapato yanayokusanywa yanakwenda kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Akizungumza jana Ikulu, Dar es Salaam baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa, alisema kwamba ni lazima nidhamu ya Serikali kwa wananchi wake iwe sambamba na viongozi na watendaji wa Serikali kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Mkuu huyo wa nchi alikuwa akizungumza ikiwa ni utaratibu wake mpya tangu alipoteua viongozi ambapo awali alikuwa akiwaapisha na kuondoka bila kusema jambo lolote.
“Nimeamua kuwateua wakuu wa mikoa nikiamini kwamba mtaniwakilisha vizuri katika mikoa yenu, napenda niwaombe mtakapowasili kwenye mikoa yenu mkitambua kwamba ninyi ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika mikoa yenu na mnatuwakilisha sisi ambao tuko huku, mkatimize wajibu wenu.
“Kukubali kwenu kuapishwa na kusaini mtakuwa mmekubali kuingia kufanya kazi na mimi, nawapa pole kwa sababu mtakwenda kufanya kazi kweli kweli kutatua kero za wananchi, haiwezekani kero inajulikana mkoani na wewe upo ukisubiri hadi aje Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au mawaziri au mimi kutatua, hiyo itajulikana kwamba mmeshindwa kazi,” alisema.
MISHAHARA HEWA
Akizungumzia juu ya uwepo wa mishahara hewa kwa wafanyakazi nchini, Rais Magufuli alisema kwa muda mrefu Taifa limekuwa likiumizwa kutokana na jambo hilo.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wakuu wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo ndani ya siku 15.
Alisema katika halmashauri nchini kuna uozo mkubwa ambapo alieleza namna walivyotuma watu kwa ajili ya kufanya utafiti katika mikoa ya Singida na Dodoma na kubaini mishahara hewa kati ya Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu.
Rais Magufuli alisema katika mikoa hiyo walifanya utafiti kwa wafanyakazi 26,900 kwenye halmashauri 14 ambapo walibaini kuwapo kwa wafanyakazi hewa 202.
“Wapo waliokuwa wakilipwa mishahara wakiwa wamekufa, wafungwa, wastaafu. Lakini 202 wote wanalipwa mishahara huku wengine 3,200 wakati kazi hiyo ikifanyika hawakufanyiwa kutokana na sababu mbalimbali ambazo ni wengine kuwa masomoni, watoro na wengine walikuwa wagonjwa,” alisema Rais Magufuli.
Alitoa mchanganuo kwamba miongoni mwa wafanyakazi 202 waliokuwa wakilipwa mishahara hewa, sita ni walioacha kazi, waliokufa na kufungwa 27, waliofukuzwa 8 na wastaafu 58 na waliokuwa likizo bila malipo walikuwa watatu.
“Ukichukua kwenye halmashauri 180 tulizonazo ukafanya hesabu rahisi ya kukokotoa, utakuta kama halmashauri zote ziko hivyo, maana yake utakuta ni jumla ya wafanyakazi 2597.4 ambao ni hewa.
“Ukikadiria kwamba kila mmoja analipwa mshahara wa milioni moja kwa mwezi na wapo ambao wanalipwa zaidi, hivyo tutakuwa tunapoteza bilioni 2.5 kila mwezi,” alisema Magufuli.
“Kuna wafanyakazi 320 ambao hawajulikani kama wapo kazini, lakini bado wamekuwa wakilipwa mishahara hali inayosababisha Serikali kupoteza mapato makubwa.
“Kila mwezi tunalipa mishahara kati ya shilingi bilioni 549 hadi 550, kati ya hiyo ipo mishahara feki. Kutokana na hali hiyo, wakuu wa mikoa nendeni mkasimamie hilo na ninawapa grace time (kipindi), ndani ya siku 15 wakurugenzi wawe wamejumlisha na wamewatoa wafanyakazi hewa katika Payroll,” alisema Rais Magufuli.
Alisema ikiwa itabainika mkurugenzi atalipa mishahara hewa atachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.
“Mshahara wa mwezi tukigundua mkurugenzi amelipa mshahara hewa ajue hana kazi na tunampeleka mahakamani. Kati ya halmashauti 14 za mikoa ya Dodoma na Singida imegundulika kuna wafanyakazi hewa 202, ninajua mawaziri mpo hapa, Waziri wa Fedha upo, komesheni wizi wa fedha.
“Nendeni mkawaambie wakurugenzi watoe wafanyakazi hewa kwani tunahitaji mapato tunayopata yaende kwa wananchi,” alisema.
ELIMU BURE
Akizungumzi suala la elimu bure, Rais Magufuli aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanakwenda kusimamia suala hilo kwa vitendo.
Alisema kutokana na hali hiyo, hivi sasa Mkoa wa Dar es Salaam umeitikia wito huo vizuri kwa kuhakikisha elimu inatolewa bure kuanzia darasa la kwanza hadi kitado cha nne.
Pamoja na hali hiyo, aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa madawati na majengo.
“Kuhusu suala la elimu bure ninajua hivi sasa Dar es Salaam imeitikia na kutekeleza suala hili, na hivi sasa wazazi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupeleka watoto shule, sasa nyinyi (wakuu wa mikoa) nendeni mkasimamie upatikanaji wa madawati na majengo ya uhakika,” alisema.
UTEUZI KUCHELEWA
Rais Magufuli alitoboa siri ya kuchelewa kuteua wakuu wa mikoa akisema kuwa alikuwa akifanya uhakiki wa kina wa kubaini kama watu atakaowateua wataweza kazi hiyo.
“Nimeamua kuwateua wakuu wa mikoa nikiamini kwamba mtaniwakilisha vizuri katika mikoa yenu, napenda niwape pole kwa sababu mtakwenda kufanya kazi kweli kweli kutatua kero za wananchi wetu.
“Ndiyo maana nilikuwa najiuliza huyo kweli ataweza, maana kama usipokuwa makini unaweza siku moja ukamfuta, kumsamehe. Lakini naamini mtaweza kazi hii na hamtaniungusha,” alisema.
AONYA SIASA
Rais Magufuli aliwataka wakuu hao wa mikoa kwenda kufanya kazi na si kutangaza siasa.
“Hamuendi kutangaza siasa, mnakwenda kufanya kazi na mkasimamie fursa kwa vijana wapate ajira,” alisema.
UTAWALA WA SHERIA
Aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanakwenda kusimamia utawala wa sheria ili wananchi watii sheria bila shuruti.
Alisema hivi wapo baadhi ya watendaji, hasa wa ngazi ya kata ambao wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi, na kama wapo viongozi wa aina hiyo wawekwe ndani ili nidhamu ya Tanzania mpya ipatikane.
“Msiogope kuchukua maamuzi magumu kama njia hii ndiyo itasaidia kujenga Tanzania mpya, nendeni mkawatumikie wananchi walio wanyonge,” alisema.
MAMLAKA YA WAKUU WA MIKOA
Rais Magufuli aliwataka wakuu hao wa mikoa kwenda kujipanga kikamilifu kwa kuhakikisha wanawachukulia sheria wale wanaokwenda kinyume.
“Nyinyi mna mamlaka ya kuwaweka watu ndani hata masaa 48, wekeni watu ndani ili wajue mnatakiwa kuheshimiwa. Tusiogope kuchukua maamuzi, nafuu uchukue maamuzi hata kama ni mabaya yatarekebika huko mbele,” alisema.
USIMAMIZI KWA MA-DC, MA-DED
Aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanakwenda kuwasimamia vizuri wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kwa kuhakikisha wanawajibika ipasavyo.
“Mabadiliko huchukua muda na lazima yaonekane, ila ni lazima tubadilike,” alisema.
ULINZI NA USALAMA
Katika maeneo ya porini, hasa mikoa ya Kagera, Katavi na Kigoma, kumekuwa na mazoea kwa wasafiri wa mabasi kusindikizwa na askari polisi.
“Haiwezekani kwa nchi ambayo imejitawala zaidi ya miaka 50, eti raia wake wanaposafiri lazima wasindikizwe na polisi, ambayo inamaanisha kwamba hakuna usalama, hivyo nimeteua watu ambao nimefikiri watasimamia wananchi wasiendelee kusindikizwa na polisi.
“Ulinzi ukaimarike na wananchi watembee katika nchi yao wakiwa salama, nitashangaa sana iwapo Meja Jenerali Mustapha Kijuu ambaye umekuwa ukisimamia jeshi la nchi kavu nchi nzima ya Tanzania, sidhani kama utashindwa kusimamia Mkoa wa Kagera na watu wakashindwa kukaa kwa amani na ninajua uwezo huo unao,” alisema Rais Magufuli.
VIJANA NA POOL TABLE
Rais Magufuli aliwataka wakuu hao wa mikoa wasimamie watu wafanye kazi, hasa vijana ambao wamekuwa wakicheza Pool table saa mbili asubuhi halafu wanaokuwa mashambani ni akina mama na wazee pekee.
“Haiwezekani vijana wawe wanashinda vijiweni wanacheza pool, wakati wazee na akina mama wapo mashambani wanalima. Kawahimizeni wafanye kazi, wasipofanya kwa hiari walazimisheni kufanya kazi.
“Watanzania hawafanyi kazi na kama hawawezi kufanya kazi kwa kuambiwa, basi watafanya kazi kwa lazima, kwa sababu kama wamezoea kukaa bila kufanya kazi, shika wapelekeni kwenye mapori wakalime kwa nguvu, akitoka huko atakuwa ameelewa kwamba asiyefanya kazi na asile,” alisema Rais Magufuli.
RUNGU TRA
Akieleza hatua ya kumwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Valentino Mlowola, alisema anataka kuona mapato yanayokusanywa yanakwenda kuwanufaisha wananchi.
MAPIGANO MOROGORO
Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli alieleza uamuzi wake wa kumwacha katika uteuzi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajab Rutengwe kuwa ni kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji ambapo kila mara wananchi hupoteza maisha.
“Morogoro watu wanauana sana ndiyo maana sikuona sababu ya mkuu wa mkoa kubaki pale. ‘Message sent and delivered’,” alisema
ZIARA YA RAIS WA VIETNAM
Akizungumzia ziara ya siku tatu ya Rais wa Vietnam, Trough Tan Sang, aliyoifanya nchini Machi 8, mwaka huu, alisema anashangazwa na taifa hilo kupiga hatua kimaendeleo licha ya kupita katika changamoto kadhaa ikiwamo mapigano na vita.
Alisema pamoja na hali hiyo, nchi hiyo ilikuja nchini katika miaka 1970 na kuchukua mbegu za mpunga, korosho na samaki jambo ambalo sasa limeipaisha kiuchumi.
Rais Magufuli alisema mbegu hizo zilizochukuliwa miaka ya 1970, zimeifanya nchi hiyo kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao hayo pamoja na ufugaji wa samaki.
“Hili nachomekea kidogo, licha ya Vietnam kupita katika changamoto kadhaa, lakini wamefanikiwa kupaa kichumi. Walikuja hapa na kwenda Mtwara kwa Mheshimiwa Dendegu (Halima) na kuchukua mbegu za korosho, leo wamekuwa wazalishaji wazuri kuliko hapa kwetu.
“Kule kuna bodi za ajabu na wananchi wanalalamika. Leo hii ndiyo wazalishaji wazuri na wakubwa wa samaki, korosho na hata kahawa duniani,” alisema.