Na Seif Abalhassan
“UJAMAA utabaki kuwa tumaini na njia pekee kwa wanyonge kujikomboa. Leo wakati maadui wa ujamaa wakieneza propaganda dhidi ya Ujamaa, tunapaswa kuulinda na kuutetea zaidi ujamaa kuliko wakati mwengine wowote ule,” – Komredi Fidel Castro Ruiz, 1989.
Cuba ni kisiwa mashuhuri zaidi ulimwenguni, ni nchi mashuhuri na ya fahari mno kwa wajamaa wote ulimwenguni. July 26, 1959 viongozi wa Kijamaa wa Cuba walifanya Mapinduzi yaliyoung'oa utawala wa Rais Baptista, na kuitangaza Cuba kuwa Taifa la Kwanza la Kijamaa huko Amerika ya Kusini.
Njia zote kuu za Uchumi wa Taifa hilo zikawekwa kwa umma chini ya usimamizi wa dola, umma wa wanyonge wa Cuba kwa pamoja ukakubaliana kujenga taifa lenye usawa na linalothamini utu wa kila mmoja wao, wakulima wa miwa vijijini wakishirikiana na wafanyakazi wa viwandani mjini kuleta maendeleo ya taifa lao.
Miaka 25 ya Mapinduzi ya Cuba ilileta mafanikio makubwa ya kiutu ulimwenguni, yakiliwezesha taifa hilo kujitegemea katika kila nyanja, likifuta ujinga kwa takribani asilimia 95, likiweza kujitegemea kwa chakula na likiwa mbele ulimwenguni katika mapinduzi ya sekta ya afya – sekta ya fahari zaidi kwa nchi hiyo. Sera ya nje ya taifa hilo nayo ilizaa matunda mno, likisaidia harakati za mapambano ya Uhuru katika nchi mbalimbali za bara la Afrika, ikipeleka na wapiganaji katika mataifa kadhaa ya Afrika.
Msingi mkuu wa Mapinduzi ya Cuba ulijengwa juu ya wananchi kujitolea, miaka 25 baada ya Mapinduzi morali wa watu wa Cuba kujitolea ulishuka sana, hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, hata sekta ya fahari ya afya ikaanza kulegalega, kukawa na ucheleweshwaji au upungufu wa ujenzi wa vituo vipya vya afya na pia kuvunjika moyo kwa watabibu kulikotokana na sababu mbalimbali za kiutawala.
Haja ya kujisaili na kujisahihisha ikajionyesha, tathmini iliyofanyika juu ya usahihi na mapungufu ya sera za Kijamaa za nchi hiyo mwaka 1984 ilisaidia mno kuainisha matatizo hayo.
Mwaka 1986, mpango maalumu wa Serikali wa ‘Kujisahihisha’ ukaanza ukihusisha kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya uongozi ya zaidi ya asilimia 50 ya Chama cha Kijamaa cha Cuba pamoja na Serikali, mabadiliko ambayo yalihusisha kuleta nguvu mpya ya vijana, wanawake na Wacuba weusi.
Mabadiliko hayo hayakuishia hapo, yalihusisha pia kuvunja minyororo ya urasimu na ufisadi, kutoa motisha na morali kwa wafanyakazi, kupeleka sehemu kubwa ya fedha za umma katika miradi yenye kuzalisha ajira zaidi, kuchochea uzalishaji na kuhamasisha watu kujitolea – msingi mkuu wa Mapinduzi ya Cuba.
Wakati Cuba wakifanya hayo, nchini mwetu Tanzania tulikuwa na matatizo kama yao tu. Mwaka 1967 tulitangaza Azimio La Arusha, mwongozo wa Kiuchumi na Kisiasa uliotoa matumaini na matarajio mapya kwa tabaka la wafanyakazi na wavujajasho wengine.
Azimio liliongea lugha ya Ukombozi wa wanyonge, likanadi usawa wa kiutu, likapinga unyonyaji wa mtu na mtu au kundi moja kulinyonya jengine na likaweka miiko ya uongozi ili kuwazuia ‘kisheria’ viongozi kutumia nafasi za uongozi kujilimbikizia mali wao binafsi na familia zao.
Azimio lilileta mafanikio makubwa sana nchini, kama ilivyo Cuba lilihakikisha njia kuu za Uchumi zinashikwa na umma kupitia dola, likafuta ada kwa ngazi zote za elimu nchini – msingi kwa ajili ya mpango wa elimu kwa wote (UPE). Mpaka mwaka 1982 kila kijiji kilikuwa na shule yake ya msingi nchini, watoto wote wakipata fursa ya kusoma bila kujali hali zao.