25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

NI MAPEMA MNO KUMFANANISHA IBRAHIMOVIC NA CANTONA

ADAM MKWEPU NA MITANDAO


NI burudani ya kutosha kumtazama mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic hasa anapokuwa uwanjani.

Kwani uhodari wake wa kulishambulia lango la timu pinzani unaweza kukufanya damu ikusisimke na kukumbuka matukio ya wachezaji hodari waliopita ndani ya klabu hiyo.

Ibrahimovic anaweza kuyarudisha mawazo ya mashabiki miaka ya 90 wakati soka la England likiwakilishwa vema na damu changa kutoka ukanda wa Kaskazini Magharibi mwa England.

Ukanda huo ndio ulikuwa ukisifika kwa kutoa washambuliaji hodari ambao walikuwa na vipawa vya kusakata soka.

Wakati huo Liverpool ilikuwa ikiwakilishwa na mshambuliaji, Dean Saunders  ambaye aliisaidia timu hiyo kuibuka na ubingwa wa Kombe la FA baada ya kufikisha jumla ya mabao 23 hiyo ikiwa mwaka 1992.

Lakini Saunders aliondoka katika klabu hiyo baada ya msimu mmoja kumalizika na kutimkia timu ya Aston Villa.

Historia ya Saunders inaweza kufanana na Ibrahimovic ndani ya msimu mmoja wa Ibrahimovic, lakini bado itakuwa vigumu kuthubutu kufanya hivyo lakini kutokana na hiki kilichotokea katika fainali ya Kombe la Ligi (EFL) inawezekana.

Baadhi ya mashabiki tayari wameenda mbali na kumfananisha mchezaji huyo na aliyekuwa nguli wa Manchester United, Eric Cantona.

Mashabiki wa Manchester United wanaona kama Cantona mpya ametokea kwenye umbo la Ibrahimovic England si kwa sababu ya idadi na aina ya mabao anayofunga, hapana, bali ni manjonjo lakini kubwa zaidi linatokana na klabu hiyo kufanya vibaya wakati ilipokuwa chini ya kocha Louis van Gaal na David Moyes.

Hauwezi kupingana na mitazamo ya wengi na kushinda hasa linapokuja suala la hamasa na imani ya mashabiki kwa kile wanachokipenda na kukishuhudia ndani ya uwanja.

Wataalamu wa mambo wanaposema shabiki wa soka hana tofauti na kichaa hutakiwi kubisha bali kufanya utafiti, hasa kwa kile alichofanya Ibrahimovic wiki iliyopita katika  mchezo wa fainali  ya Kombe la Ligi dhidi ya  Southampton katika Uwanja wa Wembley.

Zaidi ya hapo kwamba kuna dalili za awali za kufanana kwa wachezaji hao wawili; Ibrahimovic na Cantona, lakini bado unatakiwa muda wa ziada wa nyota huyo kulidhihirisha hilo.

Mbali na jambo hilo, soka lenyewe limepoteza mipaka yake na kufanya kukosekana utamaduni wa wachezaji wenye vipaji hivyo kufanya ugumu wa kufikiri kama inawezekana kuvishuhudia tena vipaji vilivyopita levo za klabu.

Lakini soka la England kila siku licha ya kuwa na mahitaji yanayofanana, linapendwa zaidi akiwapo shujaa atakayelibeba mabegani na kuliweka katika uso wa dunia.

Hilo ndilo linalotokea baada ya Cantona mpya aliposaini klabu ya Manchester United miaka michache iliyopita.

Dimitar Berbatov alitajwa kuwa Cantona mpya katika klabu hiyo ikiwa miaka ni nane imepita tangu asaini na kucheza katika timu hiyo.

Mwingine alikuwa Robin van Persie aliyekuwa akifanana na nguli huyo baada ya kucheza miezi sita ndani ya klabu hiyo.

Tofauti kidogo na wengine, Anthony Martial, alianza kufananishwa na Cantona baada ya mwezi mmoja tu.

Zaidi ya yote na jambo la kufurahisha ni pale mwaka 2013 Marouane Fellaini alivyopamba magazeti ya jiji la London kuwa nyota huyo huenda akafanana  na Cantona, hiyo ikiwa kwa mujibu wa mchezaji wa zamani wa Manchester United, Henning Berg. Lakini hakukuwa na ukweli wowote juu ya jambo hilo.

Cantona alijiunga na Manchester United akiwa na umri wa miaka 26 wakati huo wakiwapo wachezaji chipukizi kama vile David Beckham, Nicky Butt, Gary Neville na Ryan Giggs, wakiongozwa na Roy Kean.

Umri na aina ya wachezaji wanaocheza na Ibrahimovic ni jambo lingine linalofanya kuwapo kwa tofauti kubwa ndani ya klabu hiyo.

Kilichotokea kwa Ibrahimovic dhidi ya Southampton, kingekuwa na hamasa kubwa kama kingefanywa na Paul Pogba, Martial na Marcus Rashford.

Hiki ni kizazi pekee ambacho kinaweza kufanya mambo makubwa bila ya uwepo wa Ibrahimovic na bado dunia ikaweza kutambua umuhimu wao.

Jambo la kutia moyo United kwa sasa ni kwamba wana mshambuliaji ambaye  anawafanya klabu nyingine kukumbuka miaka iliyopita.

United kwa sasa wanaweza kuwakumbusha Liverpool enzi za Luiz Suarez wakati Barcelona wakikumbuka uamuzi wao wa hasara walipoamua kumtimua mchezaji huyo.

Msimu huu, Ibrahimovic ameweza kufunga mabao ambayo yameisaidia timu yake kupata ushindi na kusonga mbele ikitafuta nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya.

Kwa sasa ana mabao 15 ya Ligi Kuu, Wayne Rooney, Rashford, Memphis Depay, Henrikh Mkhitaryan, Jesse Lingard, Fellaini na  Martial kwa pamoja wamefikisha mabao 11 katika michezo yao waliyocheza msimu huu.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna dalili zozote zinazoonesha kwamba Ibrahimovic ataweza kudumu kwa muda mrefu zaidi ya kumalizia michezo 13 iliyobaki kabla ya ya ligi hiyo kumalizika.

Achana na hilo, muhimu kwa sasa United tayari wamefanikiwa kulipata taji lingine baada ya kombe la mfalme mbele ya macho ya mshambuliaji huyo hivyo mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kuongeza nguvu na kusonga mbele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles