26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ni kamatakamata

Freeman Mbowe
Freeman Mbowe

*Mbowe, vigogo kadhaa wakamatwa Mwanza

*Zitto Kabwe asakwa na polisi kila kona Dar

Na Waandishi Wetu, Dar/Mwanza

SASA ni kamatakamata tu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jeshi la polisi kuwatia mbaroni vigogo kadhaa wa vyama vya upinzani akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi waandamizi wa chama hicho.

Hatua  ya kutiwa mbaroni kwa viongozi hao  imechukuliwa siku chache baada ya jeshi hilo kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa kwa kile lilichodai sababu za intelenjesia.

Agizo hilo la jeshi la polisi lilitolewa Juni 7, mwaka huu na Kamishina wa  Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Mssanzya.

Alisema kuzuiwa mikutano na maandamano hayo kunatokana na kile polisi walichoeleza kubaini mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

Siku  iliyofuata, Mbowe aliongoza wana Chadema mjini Kahama mkoani Shinyanga kwa lengo la kufanya mkutano.

Lakini walijikuta wakitawanywa kwa mabomu ya machozi jambo ambalo lililowafanya waazimie kufungua shauri mahakamani kupinga amri hiyo ya polisi.

Taarifa iliyotolewa  Dar es Salaam jana na Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema mbali na Mbowe, viongozi wengine waliotiwa mbaroni ni Katibu Mkuu Baraza la Vijana (Bavicha),  Julius Mwita ambao wote wanatuhumiwa kusalimiana na wanachama wa Chadema kwenye ‘vijiwe’ kadhaa eneo la Igoma Centre,  Mwanza.

Wengine waliotiwa mbaroni ni Mbunge wa Tunduma,  Frank Mwakajoka,  viongozi wengine   na wanachama  ambao wote  wanashikiliwa   katika  Kituo cha Polisi Nyakato,  Mwanza……

“Hadi sasa hakuna maelezo ya sababu ya kushikiliwa kwao. Tangu asubuhi Mwenyekiti wa Chama,  Mbowe alikuwa akizunguka katika maeneo kadhaa ya  Mwanza kuwasalimia wananchi katika ‘vijiwe’  mbalimbali jijini humo,” alisema Makene katika taarifa yake.

Mbowe

Mbowe, alihojiwa kwa saa mbili katika kituo cha Polisi Nyakato Wilaya ya Nyamagana, huku akizuiliwa kutembea eneo lolote katika Jiji la Mwanza bila idhini ya polisi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, bada ya kuachiwa kutoka kituo cha polisi, Mbowe alisema katika mahojiano hayo, yaliongozwa na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO) Augustine Senga na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, polisi walimtaka kuanzia sasa kutoendelea na ziara yoyote Mwanza bila kuwasiliana na polisi.

“Polisi wamenitaka kuanzia sasa nisitoke hoteli niliyofikia bila kutoa taarifa kwao, hili nimekataa maana huku ni kutaka kunipa kifungo cha nje kama kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye, nimewajibu mimi ni kiongozi wa Taifa kama wa CCM, ninahaki ya kutembelea ofisi zangu lakini pia kama Mtanzania ninahaki ya kutembea popote,” alisema.

Mbowe alianza ziara ya kutembelaa ofisi na matawi ya Chadema katika Jimbo la Nyamagana saa 5:16 asubuhi, ambako akiwa Nyegezi baada ya kikao cha ndani, alikwenda katika mgahawa wa kituo cha Mabadi na kunywa kahawa na baadaye alitembelea ofisi za tawi la Kambarage Kata

ya Mkuyuni na kwenda kula chakula cha mchana katika mgahawa wa mama lishe ulipo Sahara kabla ya kwenda Igoma ambako alikamatwa saa 10:30, baada ya magari ya

viongozi wake kuzuiwa.

Alisema akiwa katika ziara yake amekuwa akiambatana na wasaidizi wake, walinzi na wabunge wa chama na viongozi wa kanda, lakini polisi wamekuwa akidai msafara wake umekuwa mkubwa na kwamba unahitaji kibali cha polisi jambo ambalo alilikataa.

“Mimi sifanyi mikutano,naomba polisi watambue siwezi kufanya mikutano bila ya kipaza sauti wala majukwaa, sina woga huo, tumekubaliana na zuio lao la kufanya mikutano na ndiyo maana tumekwenda mahakamani kutafuta haki yetu huko, sasa wakitaka kuzuia na shughuli za chama hilo ni jambo lingine,” alisisitiza.

Alisema dhamira ya Polisi Mkoa wa Mwanza ni kutaka kumpa kifungo cha nje na

kuonya kuwa siasa za nchi hii sasa zinaonekana kuiga za Uganda.

Alisema katika mahojiano na polisi pia wamemuagiza kuwazuia wafuasi wake

wasifike mahakamani kusikiliza kesi ambayo imefunguliwa na chama chake kupinga zuio la kutokufanya mikutano ya hadhara.

“Polisi wamenilazimisha kuwazuia wafuasi wa Chadema

wasifike mahakamani, nimesema sina mamlaka hayo maana kesi hii sijaifungua mimi kama Mbowe, bali kwa maelekezo ya wanachama ambao wameona kuna ukiukaji mkubwa wa demokrasia, hivyo wana uhuru wa kufika mahakamani kusikiliza uamuzi utakaotolewa,” alisema.

Alisema kwa kuwa kesi hiyo,inahusu ukiukaji wa demokrasia wananchi wanapaswa kufika kwa wingi kusikiliza uamuzi utakaotolewa na mahakama kwa kuwa wakati wao Chadema wamezuiliwa kufanya mikutano wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaendelea na mikutano huyo .

Kwa upande wake, RCO Senga alisema Mbowe amekuwa akifanya mikusanyiko isiyo halali kwa

kutoka na misafara mikubwa ya magari na kukutana na watu katika vijiwe mbalimbali na kwamba hatua hiyo inapingana na agizo lililotolewa na polisi.

A l i s e m a M b o w e amekuwa akihutubia watu na kuwahamaisha wafike mahakamani kusikiliza kesi, jambo ambalo halikubariki.

Juni 7, mwaka huu, Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Mssanzya, alitoa taarifa ya kuzuiwa mikutano na maandamano kwa vyama vya siasa.

Nsato alisema vyanzo hivyo vya habari vimebainisha kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya siasa.

Polisi wamsaka ZITTO

Wakati huohuo, Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amezidi kuandamwa na polisi, baada ya askari kanzu wa jeshi hilo kumvizia maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa kile kinachodaiwa wanataka kumkamata.

Sababu ya jeshi hilo kumtafuta Zitto kwa kumvizia hazijawekwa wazi, huku viongozi wa juu wa jeshi hilo wakirushiana mpira kuzungumzia suala hilo.

Mbali na kumtafuta Zitto, pia jeshi hilo lilizuia kongamano la kuchambua mapendekezo ya bajeti ya Serikali lililokuwa linaratibiwa na chama hicho, huku viongozi wake wakitajwa kuwa wasemaji wakuu katika kongamano hilo.

Taarifa za kutafutwa Zitto zilianza kusikika usiku wa kuamkia juzi, baada ya ndugu wa karibu wa kiongozi huyo kuieleza MTANZANIA kuwa baadhi ya watu waliojitambulisha kuwa ni polisi, walifika nyumbani kwao saa sita usiku wakitaka kujua kiongozi huyo alipo.

Jana asubuhi MTANZANIA lilipata taarifa ya kutanda polisi katika jengo la Millenium Tower ambako kuongamano hilo lingefanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira alisema wameshindwa kufanya kongamano kutokana na kupokea taarifa za kusimamishwa kutoka polisi.

“Tumepata taarifa kutoka kwa vijana wetu waliokuwa wanafanya maandalizi kwamba uongozi wa jengo tulilokuwa tufanyie kongamano umesema umepokea maagizo kutoka polisi kuwa wasiruhusu jambo hilo kwa sababu halina kibali,” alisema Anna.

Mtemelwa

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa alisema hadi jana jioni walikuwa hawajui Zitto alipo na kama yupo katika hali gani.

“Askari kanzu wanalinda nyumbani kwake na watu wake wa karibu… sisi kama chama tunaliambia jeshi la polisi kuwa lolote litakalotokea kwa kiongozi wetu wao watajibu kwa umma,”alisema Mtemelwa.

Hali hiyo imejitokeza ikiwa ni siku chache tangu Zitto aitwe na kuhojiwa na polisi kwa saa mbili kuhusu maudhui ya hotuba yake aliyoitoa June 5, mwaka huu kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhiem Dar es Salaam.

Polisi

Hata hivyo, gazeti lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kinondoni, Christopher Fuime kudhibitisha taarifa hiyo, lakini alijibu hana taarifa za suala hilo na anayeweza kulizungumzia ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishana Simon Siro.

Lakini Kamishna Siro, alipotafutwa alisema atafutwa Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Advera Bulimba.

Advera alipotafutwa alisema kiongozi mwenye dhamana ya kulizungumzia ni Kamanda Siro, jambo ambalo hadi tunakwenda mitamboni lilikuwa bado halieleweki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles