Na Sheila Katikula, Mwanza
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) mkoani Mwanza,  Jarlath Mshashu amesema kwa mujibu wa kalenda yao mwaka jana wametoa kadi za bima ya afya  zaidi ya elfu 36 kwa wanaume 18,261 na wanawake 18,207.
Amesema hayo wakati akizungumza na  waandishi wa habari ofisini kwake alisema zoezi hilo ni endelevu  kwani lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anakata bima hiyo ili aweze kupata matibabu kwa urahisi pindi anapohitaji matibabu.
Alisema kila mwananchi  anawajibu wa kukata  kadi ya bima za afya  ili waweze kutibiwa  hospitalini  na kuepuka changamoto ya  kutumia dawa bila kupewa maelekezo ya wataalamu wa afya.
“Nawaomba wananchi waache mazoea ya kutumia dawa bila kupima kwani kuna baadhi ya  watu wakijiskia wanaumwa  anaenda kununua dawa kwenye duka la dawa bila kupima kwani kufanya hivyo siyo vizuri  ni vema  wakate kadi ya bima  ya afya ambayo itamsaidia muda wote utakapokuwa unaumwa.
“Inasikitisha kuona wananchi waliowengi wanajitibu kwa mazoea ya kwenda kwenye maduka ya dawa na kununua dawa ambazo haziendi kutibu ugonjwa ulioko ndani ya mwili na kusababisha maradhi mengine yanayoweza kupelekea kuugua na kupoteza nguvu kazi katika jamii,” amesema Mshashu.
Mushashu aliongeza kuwa kutumia kadi ya mtu mwingine ni kosa la jinai kwani ni uhujumu uchumi wa fedha za Serikali ni vema kila mtu atumie kadi yake ili aweze kupata matibabu bila usumbufu.
Aliongeza kuwa NHIF inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kujiunga na mfuko huo kwani mwaka jana walizunguka kwenye kata mbalimbali sanjari na kutoa elimu kwenye nyumba za ibada 50 zilizopo jijini hapa.
Amesema zaidi ya wanachama 812 walijiunga kutoka kwenye vyama vya ushirika AMCOS wilaya ya Magu na Sengerema ambapo wanachama wengi wameelimika na kujiunga kwa wingi pamoja na kulipia familia zao ili kuondokana na usumbufu wa kupata matibabu pindi wanapougua.
Mshashu amesema kwa robo mwaka iliyopita kwa mwaka wa fedha walitoa elimu ya Fao  la Ushirika kwenye vyama vya msingi vya ushirika vya wilayani Sengerema na Magu kwenye AMCOS 20  kwani zaidi ya wanachama 1,200 walipewa elimu ya kujiunga na mfuko huo kupitia  ushirika afya.Â
Alisema baada ya kutoa elimu kwenye vyama vya ushirika zaidi ya wanachama 813 walijaza fomu za kujiunga na mfuko huo kwani hivi karibuni wanatarajia kupewa kadi zao ili waweze kunufaika huduma hiyo.
“Fao hili la ushirika afya linawalenga wakulima waliojiunga na vyama hivyo kwani gharama yake ni 76,800 kwa mwaka kwa mtu mmoja naomba wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi  ili waweze kujiunga na mfuko huu wa bima ya afya,”amesema Mshashu.