25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NGUVU YA UKABILA KUAMUA MATOKEO YA URAIS NASA, JUBILEE?

 

 

Na JOHANES RESPICHIUS,

AGOSTI 8, mwaka huu, ni siku ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya, hivyo Wakenya wanatarajia kumchagua kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo pamoja na wabunge.

Uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa na mnyukano mkali kati cha chama tawala cha Jubilee dhidi ya muungano wa vyama vya upinzani nchini humo wa National Super Alliance (NASA).

Zikiwa zimebaki siku 102 tu kabla ya uchaguzi, NASA inaamua kutaja kikosi chake cha maangamizi cha watu watano ili kumtoa Ikulu Rais Uhuru Kenyatta na chama chake cha Jubilee, ambapo inamteua Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, kuwa mgombea wa urais.

Naye kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka, ameteuliwa kuwa mgombea mwenza. Kiongozi wa chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi, nafasi ya Waziri Mkuu mratibu wa shughuli za serikali, huku kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetangula, atakuwa Naibu waziri mkuu mratibu wa uchumi na kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM), Isaac Ruto, atakuwa Naibu Waziri Mkuu atakayesimamia utawala na huduma za jamii.

Ni dhahiri kwa ushirika huu wa NASA wapinzani wa Kenya wamejipanga kuchukua nchi, hasa kutokana na jinsi walivyopanga safu zao za uongozi, kuanzia ngazi za juu ambapo kila kiongozi wa chama amepata nafasi ya juu katika Serikali inayotarajiwa kuundwa baada ya Agosti 8, kama watakuwa wamefanikiwa kushinda kwenye uchaguzi huo.

Hali hii ndiyo walau inaweza kunipa matumaini kwamba upinzani wa Kenya unaweza kukinyima kura chama cha Jubilee, lakini siwezi kujihakikishia kwa asilimia zote kwasababu muunganiko wa NASA hauna tofauti na ule wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kwa hapa Tanzania, wengi waliokuwa wanaunga mkono vyama vya upinzani walikuwa na matumaini makubwa ya kukiangusha chama tawala, CCM, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, baada ya vyama vya Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD kuungana na kuunda Ukawa.

Ukawa ilianza kubadilika mara tu baada ya mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, kupeperusha bendera ya umoja huo katika uchaguzi mkuu ambapo hali ya kutoelewana ilianza baina ya viongozi, baadhi wakikubaliana na uamuzi huo na wengine wakishindwa kukubaliana.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya viongozi waandamizi wa vyama washirika kuamua kuachia ngazi na hata wengine kujivua uanachama kuhamia vyama vingine, hususan CCM, hivyo kufanya Ukawa iyumbe mpaka kupelekea kushindwa uchaguzi.

Pia ikizingatiwa kuwa Kenya si muunganiko wa kwanza wa vyama vya upinzani ili kukiondoa chama tawala, kwani imeshuhudiwa miunganiko mbalimbali, lakini Raila Odinga amekuwa akishindwa chaguzi zote.

UCHAGUZI 2007

Uchaguzi wa mwaka 2007 ulifanyika kwa kutumia katiba mpya ambayo ilipiganiwa tangu 2002 na wanasiasa kaliba ya Raila Odinga, Mwai Kibaki, Kalonzo Musyoka walijitoa chama cha KANU na kuunda umoja wa NARC kumpinga Rais Mstaafu, Daniel Arap Moi, aliyekuwa akimpigania Uhuru Kenyatta kuwa rais kupitia KANU. Vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007 zilisababisha machafuko makubwa yaliyochangia uvunjifu wa amani.

Hata hivyo, kwenye mapambano ya kupatikana katiba mpya, ilishuhudiwa mfarakano kati ya Odinga (aliongoza Umoja wa Chungwa-ODM) na rais wake, Mwai Kibaki (aliongoza Umoja wa Ndizi), ukawa mwisho wa uimara wa NARC.

Aidha, ukatokea mtikisiko wa kisiasa ndani ya chama cha ODM. Je, kutokana na kuvunjika NARC hadi kuyumba kwa chama cha ODM, je, Raila Odinga amejifunza lolote?

UCHAGUZI 2013

Katika uchaguzi huu, Raila Odinga aliingia akiwa anatoka kuwa waziri mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa, iliyoongozwa na Mwai Kibaki. Nafasi ya waziri mkuu ilianzishwa ili kuleta mshikamano na umoja kati ya chama cha PNU cha Mwai Kibaki na kile cha ODM cha Raila Odinga.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2013, Raila Odinga akiwa na makamu wake, Kalonzo Musyoka, walipambana na Uhuru Kenyatta na William Ruto, ambao kipindi hicho walikuwa watuhumiwa wa machafuko ya uchaguzi wa mwaka 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya binadamu (ICC).

Licha ya umahiri mkubwa, Raila Odinga hakufua dafu mbele ya wanasiasa Uhuru Kenyatta na William Ruto. Sababu kubwa ilidaiwa siasa za kikabila zilizopo Kenya, ambapo makabila ya Kikuyu (Uhuru Kenyatta) na Kalenjing (William Ruto) yalitamka waziwazi kuwa hayatampigia kura ‘Mjaluo’ (Raila Odinga).

Hii ni mojawapo wa sababu ya kushindwa kwake, pamoja na kudhoofika ODM kufuatia wanasiasa mbalimbali kujitoa. Jingine ni madai ya wizi wa kura katika mfumo wa uhesabuji wa Tume ya uchaguzi. Raila aliridhia kushindwa.

UCHAGUZI 2017

Mwaka huu Raila Odinga amefanya juhudi kubwa kuhakikisha Tume Huru ya Uchaguzi inakuwa na uwazi, uhuru na haki. Ili kufanikisha hayo, amewahamasisha wananchi kuandamana kila kona ya Kenya na walihakikisha matakwa yao yanatekelezwa na serikali ya Uhuru Kenyatta.

Maandamano yasiyo na kikomo yalichangia suala hilo kufikishwa mahakamani, ambapo serikali iliwasilisha pingamizi. Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali pingamizi la srikali. Sasa uchaguzi wa mwaka 2017 umekuja, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wameonyesha dhamira ya kuibwaga serikali ya Jubilee.

Kwenye duru hili, Raila na Kalonzo wamekuja kwa mgongo wa kutaka kuondoa ukabila nchini humo, ambao kwa muda mrefu umekuwa tatizo ambalo limekuwa likileta machafuko.

Aidha, wanataka demokrasia, kulinda maslahi ya Wakenya, kupambana na ufisadi, kuahidi mabadiliko katika sekta ya afya, elimu, ajira na kuondoa umasikini.

Ahadi za Raila Odinga na Kalonzo ni nzuri kwa masilahi ya Wakenya, lakini swali ni je, Wakenya wenyewe wameshakuwa na utashi wa kuamua kuachana na ukabila ambao unalitesa taifa hilo tangu kupata uhuru? Kama jibu ni ndiyo, NASA wameula, kama hapana wembe unaweza kuwa ni ule ule, kwani ukiangalia makabila ya Kenyatta na Rutto ndiyo yenye nguvu zaidi nchini humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles