25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Nguvila aagiza ujenzi wa shule kukamilika kwa wakati

Na Renatha Kipaka, Bukoba

Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila amewataka mafundi na kamati za usimamizi wa ujenzi kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa shule hizo Machi 15, mwaka huu.

Nguvila ameyasema hayo leo Februari 16, baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule tatu mpya za sekondari zinazojengwa katika kata za Karambi, Mushabago na Mafumbo kwa fedha za mradi wa SEQUIP.

Akizungumza katika ziara hiyo Nguvila amewasihi mafundi kuhakikisha kila chumba kinakuwa na mafundi nane na wasaidizi nane ili kazi iishe haraka na kuwezesha wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kwenda kusoma shule za jirani kuhamia katika shule zao mpya kama ambavyo lengo la ujenzi wa shule hizo ulivyokusudia.

“Tarehe 15 mwezi wa tatu ujenzi uwe umekamilika na baada ya likizo fupi ya Pasaka watoto wote walio katika shule mama/shule jirani watahamia katika shule mpya zilizojengwa ndani ya kata zao. Wekeni jenereta, kazi ifanyike masaa 24 na ikamilike kwa ubora,” amesema Nguvila.

Aidha, amewasihi na kuwasisitiza mafundi wakuu endapo kuna fundi anashindwa kufikia malengo wanayowapangia wawaondoe na kuleta mafundi wengine kwani wanaohitaji kazi ni wengi na sio suala la kuwabembeleza na matokeo yake kukwamisha kazi.

Amesisitiza kuwa kamati za ujenzi kusimamia na kuhakikisha vifaa vyote vya ujenzi kuanzia mchanga, nondo, saruji na tofari vinakuwepo katika eneo la ujenzi kabla ya mvua hazijaanza kunyesha ili kuondoa visingizio vya mafundi kutofanya kazi kwasababu ya kutokuwepo kwa vifaa vya ujenzi.

Sambamba na hayo amewasihi pia kuhakikisha malipo ya mafundi na vibarua yanafanyika kwa wakati kwa kila hatua ya ujenzi wanayokuwa wamefikia ili kuwapa moyo wa kufanya kazi na kuwezesha kazi kukamilika kwa wakati na kuonesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya kata ya Mafumbo, huku akiwataka mafundi kuendelea na juhudi ili kukamilisha kazi kwa wakati.

Mhandisi wa Ujenzi wilaya ya Muleba, Mhandisi Zephania Chacha, amewataka mafundi kufanya kazi kwa kuzingatia mipango kazi yao, kujenga kwa viwango na ubora unaotakiwa na kamati za ujenzi kusimamia ipasavyo ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati.

Kila shule imepokea Sh milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, vyumba vitatu vya maabara, chumba kimoja cha ICT, maktaba, jengo la utawala na matundu 20 ya vyoo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles