NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
IDADI kubwa ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 18, hasa wa kike, wanafanyiwa vitendo vya ngono katika ngoma za usiku maarufu kama ‘vigodoro’.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Watoto na Walemavu, Sihaba Nkinga, alisema hayo juzi alipozungumza na MTANZANIA Jumapili, saa chache baada ya kumalizika kwa semina ya siku moja ya waandishi wa habari kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Alisema watoto wengi waliohojiwa na maofisa wa wizara hiyo walikiri kufanyiwa vitendo hivyo kwenye vigodoro hali iliyowasababishia wengine kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo.
“Hali ya ukatili wa kijinsia nchini ni mbaya, wanawake wengi na watoto wanafanyiwa ukatili, lakini mwaka 2009 tulifanya utafiti na matokeo hayo yalitoka mwaka 2011, watoto wengi waliohojiwa walikiri kufanyiwa vitendo vya ngono kwenye vigodoro.
“Tuligundua pia zipo baadhi ya mila na desturi ambazo watu wamezishikilia ambazo ni kikwazo katika mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni, kuna familia nyingine zina umasikini ambao nao unachochea tatizo kwani familia zinaona watoto wa kike kama kitega uchumi chao,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo jamii bado inahitaji elimu zaidi ili kupambana na ongezeko la idadi ya ndoa na mimba za utotoni na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Leo hii tunalalamika kuna mmonyoko wa maadili lakini kiukweli suala hilo ni matokeo ya ukatili ambao wengi walifanyiwa wakati wa utotoni.
“Takwimu zinaonyesha kuwa watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili, lakini jamii haifuatilii, kwa mfano utafiti wa mwaka 2010 unaonyesha asilimia 39 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 30 wanafanyiwa ukatili.
“Na kati ya watoto saba, mmoja anakuwa amefanyiwa ukatili, hivyo tunahitaji ushirikiano wa karibu wa kila mmoja kufikisha ujumbe kwa mwenzake kwamba hali ni mbaya,” alisema.