25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ngeleja agoma kung’oka

ngelejaSHABANI MATUTU NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja, ameendelea kushikilia msimamo wake kutojiuzulu nafasi yake hiyo kama ilivyoelekezwa katika maazimio nane ya Bunge.
Mbali na Ngeleja, katika azimio hilo la Bunge linataka Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, waondolewe katika nafasi zao kutokana na kufaidika na mgawo wa fedha za Escrow.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Utawala, Gosbert Blandes, alisema hakuna kanuni za Bunge zinazoelekeza utekelezaji wa maazimio hayo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Ngeleja mwenyewe, aliyetakiwa na waandishi wa habari kuelezea msimamo wake ambapo alijibu kwa kifupi kwamba alichosema Blandes ndivyo ilivyo.
“Sina cha kuongeza zaidi, kwani alichokisema Makamu Mwenyekiti ndiyo uamuzi wangu na kamati,” alisema kwa kifupi Ngeleja na kuingia ndani ya gari lake.
Taarifa ya Blandes ilijikita zaidi katika kumtetea Ngeleja kwa kusema kuwa kamati haijaona sheria wala kanuni zinazowaongoza namna ya kumng’oa mwenyekiti pindi anapotuhumiwa katika vitendo vya kifisadi.
“Ngeleja amekuwa akiongoza vikao vya Kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge tangu vilipoanza Januari 13, ambapo katika kikao chake cha kwanza aligusia suala la kutimiza maazimio ya Bunge ambapo baada ya mjadala mrefu ilibainika kutokuwapo kwa sheria wala kanuni zilizoelekeza namna ya kuwawajibisha watuhumiwa.
“Kama mnavyojua kamati zote ziko chini ya ofisi ya Spika, hivyo kama Ngeleja angetakiwa kujiuzulu, Spika ambaye ndiye msimamizi wa utekelezaji wa maazimio hayo kwa upande wa wenyeviti wa kamati, angekuwa ameshatoa mwongozo.
“Lakini hadi sasa hakuna mwongozo wowote uliotolewa kutoka kwa ofisi ya Spika Anna Makinda wala Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah, unaomtaka mwenyekiti kujiuzulu,” alisema.
Alipotakiwa kuelezea kama maazimio ya Bunge yanatenganishwa na Spika, ambaye ni msimamizi mkuu wa mhimili huo, Blandes alisema wanachosubiri ni uamuzi wa Spika kwa sababu alishasema tangu mwanzo nikuwa suala la wenyeviti atalishughulikia mwenyewe kwa sababu lipo chini yake.
“Kama ilivyokuwa kwa wale majaji wanaotuhumiwa kuhusika katika ufisadi huo, Jaji Mkuu Othman Chande alisema kazi hiyo ataishughulikia, ndivyo ilivyo kwa Spika na wenyeviti wa Kamati ya Bunge,” alisema.
Aliongeza kuwa suala la kelele kuhusu kutolewa kwa Ngeleja limekuwa likipigwa nje, lakini wajumbe wa kamati hiyo wote wameridhia kuongozwa na mwenyekiti huyo.
Wakati Blandes akisema hayo, juzi Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, wakati akizungumza na gazeti hili alisema kuwa tangu vilipoanza vikao Januari 13, mwaka huu, Ngeleja amekuwa akiendesha vikao vya kamati, licha ya wajumbe kumtaka akae pembeni.
Lissu alisema alikuwa miongoni mwa wajumbe waliomshauri Ngeleja kuachia kiti hicho kama maazimio manane ya Bunge yalivyowataka wenyeviti waliotajwa kuhusika katika uchotwaji wa Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ambapo yeye alipewa mgawo wa Sh milioni 40.4 kinyume cha sheria.
Lissu alisema pamoja na kumshauri kuachia ngazi, lakini Ngeleja aligoma kwa madai kwamba akifanya hivyo ataonesha wazi kuwa alihusika katika wizi huo.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alipotafutwa jana na gazeti hili, yeye wala Naibu wake, Job Ndugai hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Juhudi za kuwatafuta viongozi hao bado zinaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles