TEL AVIV, ISRAEL
WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amefuta ziara ya mwenzake wa Ukraine baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kupiga kura kuamua ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi usitishwe.
Waziri Mkuu wa Ukraine, Volodymyr Groysman, alikuwa akitarajiwa kuitembelea Israel keshokutwa, lakini Netanyahu ameamrisha safari hiyo ifutwe baada ya Ukraine kuunga mkono kura hiyo.
Umoja wa Mataifa ulipiga kura kuitaka Israel kusitisha ujenzi huo kwa kura 14.
Marekani, ambaye ni mshirika wa karibu wa Israel haikupiga kura wala kulipinga azimio hilo kwa kura yake ya turufu na hivyo kusaidia kupita kirahisi kwa muswada huo.
Hata hivyo, Netanyahu amesema hatoliheshimu azimio hilo, na ameiamuru wizara yake ya mambo ya nje kutathmini upya uhusiano wake na taasisi za Umoja wa Mataifa.
Aidha amewaita na kuwaonya mabalozi wa nchi zinazowakilishwa katika UNSC.
Mabalozi wa Ufaransa, Uingereza, Urusi, China na Hispania ni miongoni mwa walioitwa
Aidha alisema Israel inasubiri kwa hamu kufanya kazi kwa ushirikiano na Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump, kukabiliana na kile alichodai madhara ya azimio hilo.