Na Faraja Masinde, Tabora
Wazazi mkoani Tabora wameeleza namna ambavyo nenda, rudi ilivyokuwa ikisababisha watoto wao kushindwa kusajiliwa na hivyo kukosa vyeti vya kuzaliwa.
Wakizungumza na MTANZANIA DIGITAL mapema leo Juni 3, 2022 katika viwanja vya Chipukizi, Kanyenye Manispaa ya Tabora kabla ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto waliochini ya miaka mitano kwa mkoa huo, baadhi ya wazazi hao wamesema kuwa usumbufu huo ndio chanzo cha watoto wengi kukosa vyeti.
Esther Emmanuel ambaye ni mkazi wa Tabora, Rwanzali amesema kuwa amefika kufuatilia cheti cha mtoto wake baada ya kuzungushwa kwa muda mrefu tangu mtoto wake akiwa na miezi mitatu.
“Mimi leo nimefika hapa kwa ajili ya kufuatilia cheti cha mwanangu, tangazo ninalo nimesumbuka sana nilishaenda hadi kwa Mkuu wa Wilaya nazungushwa naambiwa njoo kesho…njoo kesho.
“Hela nimeshalipa 3,500 nililipia benki lakini kadri ninavyoenda ndio usumbufu unazidi, nilianza kuomba cheti mtoto wangu akiwa na miezi mitatu lakini nenda rudi nenda rudi hadi leo ninavyozungumza na wewe ana mika minne, kwa kwali hili lilikuwa linatukatisha sana tamaa,” amesema nakuongeza kuwa:
“Lakini baada ya jana kupata tangazo kuwa kuna mpango wa vyeti hapa nimeamka asubuhi kutokea Vizigo, hadi wenzangu wakaniambia unaenda wapi nikasema nafuata cheti cha mtoto, wakaniambia nitazungushwa tu kama ilikuwa kawaida, nikawajibu hakuna.
“Sasahivi nina mshukuru mama yetu Rais Samia Suluhu kwa hiki alichokifanya, kwani imeondoa usumbufu na hapa nawapigia simu nao walete watoto wao,” amesema Esther.
Upande wake, Chausiku Bakari ambaye ni mama wa watoto mapacha Sumaiya na Abdul amesema kuwa awali kulikuwa na urasimu mkubwa hatua ambayo imenyima watoto wengi vyeti vya kuzaliwa.
“Leo hapa wazazi tunaonekana kama wazembe lakini ukweli nikwamba baadhi ya viongozi wetu waliokuwa wamepewa mamlaka ya kusajili na kutoa vyeti kwa watoto wetu ndio walikuwa kikwazo kwa wengi.
“Ilikuwa nisajili watoto wangu mapema lakini kulikuwa na usumbufu sana ukienda kwenye ofisi za watendaji unaambiwa mara nenda huku sijui kule.
“Kama hiyo haitoshi, gharama badala kuwa Sh 3,000 ukifika huko unazungushwa unaombwa Sh 10,000 mambo ambayo yalitukatisha wengi tamaa, tunashukuru serikali kwa uamuzi huu, huu ni mpango mzuri sana ambao naamini kwamba kila mtoto atapata haki yake ya kusajiliwa,” amesema Chausiku.
Nae, Michael Dismas amesema kuwa anafurahia kuja kwa mpango huo kwani umesadia kuwahamasisha wanaume ambao walikuwa wazito kushiriki katika shughuli za maendeleo ya watoto wao.
“Kwa kweli hapa leo nina amani mwanangui sasahivi naweza kumuandikisha shule bila wasiwasi kwani nimeweza kufanikisha changamoto iliyokuwa imanikwamisha kwa kipindi kirefu.
“Niwahimize wanaume wenzangu ambao bado wanajishauri kuacha uzembe na waamke mara moja waje wawasajili watoto wao na siyo kusubiri kina mama tu ndio wafanye hivyo,” amesema Dismas.
Mkakati wa Mkoa wa Tabora
Jonathan Magoti ni Afisa Msajili kutoka RITA Mkoa wa Tabora ambapo amesema kuwa mpango huo wa kusajili watoto waliochini ya umri wa miaka mitano ambao umezindualiwa leo Juni 3, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makongo, unalenga kupata taarifa sahihi za watoto wanaozaliwa ili kuwa na uhakika wa taarifa sahihi kuanzia pale anapozaliwa hadi pale mfumo mwingine utakapomhitaji.
“Mfumo huu pamoja na mambo mengine unaondoa udanganyifu wa taarifa za mtoto tangu anapozaliwa hadi akiwa na miaka mitano.
“Hii inahusisha kujua majina yake, alizaliwa lini na wapi, huu ndio mwanzo wa taarifa ili mifumo mingine ikiwamo NIDA iweze kuchukua taarifa zake moja kwa moja pale atakapofikisha umri wa miaka 18,” amesema Magoti.
Vigezo vya kusajiliwa
Akizungumzia vigezo vya hadi mtoto kusajiliwa na kupata cheti Magoti amesema kuwa kwanza lazima awe na kilelezo kinachoonyesha tarehe ya kuzaliwa kama kadi ya Kliniki au tangazo la kuzaliwa mtoto.
“Pia kadi ya ujauzito wa mama au cheti cha ubatizo kwa mazingira ambayo itatubidi kama hakuna namna nyingine huku akiongeza vilelezo vingine shiriki.
“Mzazi wake mmoja lazima awe na namba ya kitambulisho cha nida aliyoandikisha kwa ajili ya kumtambua na iwapo hatakuwa nayo basi ni wazi kuwa hatakuwa Mtanzania,” amesema Magoti.
Katika hatua nyingine Magoti amesema kuwa ndani ya siku hizo 12 tangu kuzinduliwa kwa mpango huo mkoani Tabora ni kampeni ya kusajili watoto wote waliozaliwa ndani ya mipaka ya Tanzania Bara kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya muda wa siku 12 kuisha watoto watakaosajiliwa ni wale waliko ndani ya siku 90 tu ndio watakaopata huduma hii katika vituo vyote vya tiba na ofisi za watendaji wa kata wote.
“Hii inamaana kwamba tumetoa madaraka kutoka Serikali kuu kwenda kwa Mkurugenzi ambaye ana wananchi, hivyo vyeti hivyo hazitakuwa na ukomo,” amesema.
Wazazi, udanganyifu ni changamoto
Amesema tangu kuanza kwa zoezi hilo mapema Juni 3, changamoto kubwa imeonekana kuwa kwa wazazi ambapo baadhi hawana taarifa za watoto wao huku wengine wakiwa siyo raia wa Tanzania.
“Adha, tunayoipata ni wazazi au walezi kwani wengine hawana taarifa kamili ambazo zinamhusu mtoto na hata yeye mwenyewe kwani kuna baadhi ya watoto wanalelewa na bibi au babu hivyo hawa taarifa kamili za watoto.
“Pia kuna udanganyifu wa wazazi ambao wamezaliwa nje ya nchi lakini hataki kuonyesha kuwa amezaliwa Tanzania jambo ambalo siyo kweli, kwa hiyo tunajaribu kufuatilia kwa karibu ili tuweze kupata taarifa sahihi na katika hili tunawashirikisha pia wenzetu wa Uhamiaji ili kazi iwe nyepesi.
“Kwa hiyo tunasaidiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa tunaowasajili ni wale tu ambao wanastahili kusajili,” amesema Magoti.
Kwa mujibu wa Magoti, kwa mkoa wa Tabora mpango huo unalenga kusajili watoto 500,000.
Mpango huo unaratibiwa na Wakala wa Serikali wa Usajili, Ufilisi na Udhamini(RITA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF), Ubalozi wa Canada nchini Tanzania na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya TIGO.