Na MWANDISHI WETU-GEITA
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Vedast Makota amewataka wawekezaji kuzingatia sheria zinazosimamia uhifadhi wa mazingira wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kila siku.
Makota aliyasema hayo jana mkoani Geita, katika ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za uwekezaji.
“Masuala ya uwekezaji ni muhimu kama serikali inavyosisitiza, lakini tunawataka wawekezaji wasimamie sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 ili shughuli za uzalishaji uchumi zizingatie masuala ya mazingira,” alisema Dk. Makota.
Novemba 30, 2017 mvua kubwa ilinyesha mkoani Geita na kusababisha bwawa linalohifadhi mabaki ya udongo wenye kemikali zilizotokana na shughuli za uchenjuaji madini ya dhahabu katika mradi wa kampuni ya Nyarugusu Mine Ltd lililopo Kijiji cha Ziwani, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita kubomoka.
Baada ya tukio hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Malongo walifanya ziara kukagua uharibifu huo.
“Tumechukua sampuli za udongo, mazao kama mahindi na viumbe hai wakiwemo samaki na chura walioathirika ili tukapime kwenye maabara kupata hali halisi kwa namna gani maeneo haya yameathirika,” alikaririwa akieleza Dk. Makota.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyarugusu Mine Limited, Fred Masanja alisema wanatambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa ajili ya afya za wanadamu lakini tukio la kubomoka bwawa la kuhifadhia udongo wa uchenjuaji madini lilitokana na mvua kubwa, hata hivyo kwa sasa wameweka mikakati madhubuti ili lisitokee tena.