Na ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema mwenendo wa Bunge umefika pabaya kwa kuwa baadhi ya wabunge na viongozi wa Bunge hawashirikiani.
Kutokana na hilo, amesema kikao kijacho cha Bunge kinachotarajia kuanza Septemba 6 mwaka huu, lazima kuwe na majadiliano kati ya Spika na Naibu Spika, wenyeviti wa Bunge pamoja na wabunge wa upinzani.
Pamoja na hao, alisema kuna haja ya kuwashirikisha maspika wastaafu ili mwafaka uweze kupatikana.
Ndugai alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana katika mahojiano yaliyorushwa na Kituo cha Luninga cha Azam kupitia kipindi cha Funguka kilichoongozwa na Mtangazaji mkongwe nchini, Tido Mhando.
“Katika Bunge hili tuna malengo mengi ikiwapo changamoto ya kujenga Bunge moja na si vipande vipande. Kwa sasa ushirikiano umepungua bungeni, yaani kuna uvyama na migogoro imezidi, hii hali haiwapi raha Watanzania.
“Uwepo wa misukosuko hiyo si kweli kwamba imesababishwa na mimi kutokuwapo bali hali hii imeanza muda kidogo hata wakati wa Makinda (AnneMakinda, Spika mstaafu) akiwa Spika ambapo wabunge walikuwa wakigoma na kutoka nje.
“Enzi hizo baadhi yao walikuwa hawahudhurii vikao, walikuwa watoro na wengine walikuwa hawahudhurii vikao vya kamati za Bunge.
“Ili kuondokana na hali hii, tumejitahidi kutoa semina kwa kuwafundisha kanuni, lakini kila baada ya uchaguzi, tunapata changamoto kubwa kama hii ya sasa,” alisema Ndugai na kuongeza.
“Kwa mfano, wabunge ambao hawajarudi katika Bunge hili ni asilimia 70 na wapya ni asilimia 70 na hawajui kanuni.
“Yaani waliopo sasa ukiwaelekeza na wakaanza kuelewa, baadaye wataondoka na watakuja wengine wapya baada ya uchaguzi kufanyika,” alisema Spika Ndugai.
Ndugai ambaye alikuwa akitibiwa nje ya nchi kwa kipindi cha miezi miwili, alisema kwa sasa jambo ambalo linamsumbua kichwa ni namna ya kufanya maridhiano baina ya pande zinazovutana.
Katika maelezo yake, kiongozi huyo wa Bunge alisema anaumia kichwa pindi anapofikiria namna ya kutatua mgogoro uliopo bungeni kwa kuwa umeshafika katika hali asiyoridhishwa nayo.
“Wakati wa Bunge la Katiba, kanuni zilimpa Mwenyekiti wa Bunge kuunda kamati maalumu ya kutatua jambo fulani, yaani kamati ya maridhiano.
“Lakini, katika Bunge letu hili, kanuni haziruhusu hilo, ndiyo maana nafikiria tuazime uzoefu huo wa Bunge la Katiba kwa kuwa na kamati ya aina hiyo,” alisema.
Akizungumzia wabunge wa upinzani kutoshiriki vikao vya Bunge, alisema suala hilo lilimuumiza, lakini aliona ni mwendelezo wa tabia yao kwani hata wakati Rais mstaafu, Jakaya Kikwete anazindua Bunge enzi zake, walitoka nje.
“Hata wakati Rais Magufuli anazindua Bunge hili la 11, walitoka nje. Kanuni zetu haziwazuii kusimama na kutoka nje, lakini hili la sasa limezidi, yaani ni jambo ambalo halipendezi.
“Kwa hiyo, kwenye kikao cha Septemba tutajaribu kukaa mezani ili kuangalia maeneo ambayo sisi viongozi labda tunakosea ili tuone namna ya kurekebisha,” alisema.
NAIBU SPIKA NA UKAWA
Alipoulizwa kitendo cha Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kuongoza Bunge vikao vyote, Spika alisema haoni tatizo kwa sababu uongozi ndio unaopanga nani akae kwenye kiti.
Pamoja na hayo, alisema wabunge wa upinzani wanatakiwa kupeleka malalamiko yao katika kamati ili yatatuliwe kwa amani.
“Siku zote ninawatia moyo wabunge, kwamba linapotokea tatizo lolote ni vema tukae na kulirekebisha kwani haipendezi kukaa bungeni na wageni wapo, baadaye wabunge wanatoka nje,” alisisitiza.
Pamoja na malalamiko yanayotolewa na wabunge wa upinzani, Ndugai alisema baadhi ya wabunge hao wamekuwa wakijihisi kuwa wanaonewa kutokana na mazingira waliyotoka.
“Baadhi yao hadi wanafika bungeni, wanakuwa wamepitia matukio mengi mitaani, yaani wengine huwa wameshalala selo kidogo. Kwa hiyo, wanapofika bungeni, subira inakuwa ndogo, akiguswa kidogo anaanza kusema hawa wameanza tena,” alisema.
Wakati huo huo, aliwataka wabunge wa Upinzani waendelee kuwa na imani na Dk. Ackson kwa kuwa Bunge linaendeshwa kwa kanuni.
VIJEMBE
Akizungumzia kuhusu wabunge wa CCM kurusha vijembe baada ya Ukawa kutoka bungeni, alisema hilo nalo si jambo jema.
Kutokana na hali hiyo, alisema suala hilo atalikemea kwa wabunge wa CCM ili lisijirudie kwa kuwa linajenga chuki na uhasama.
WABUNGE CCM KUTOADHIBIWA
Alipoulizwa kuhusu wabunge CCM kutopewa adhabu, alisema hakuna upendeleo kwa kuwa kila anayevunja kanuni anaadhibiwa. Aliahidi pia atarudisha nidhamu ya Bunge kwa wabunge wote kuacha utoro, lugha zisizo za staha, vijembe na matusi.
AWASHAURI VIONGOZI WA BUNGE KUWA WAVUMILIVU
“Bunge hili lina wabunge wapya wengi hivyo ilibidi viongozi tuwe na uvumilivu mkubwa na kuchukuliana kukubwa ili kuwapa uzoefu wabunge wetu, lakini kwa hatua tuliyofikia hatuwezi kuendelea hata kidogo,”alisema.
LUGUMI KUPITA KIULAINI
Alipoulizwa juu ya kitendo cha wabunge machachari wa upinzani kuadhibiwa kama sehemu ya mkakati wa kupitisha kiulaini mambo ambayo walikuwa wakiyapigania kama sakata la mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi, Spika Ndugai alisema mtazamo huo si sahihi kwa kuwa suala la lugumi halijaisha kwa kuwa imeundwa timu ya ukaguzi kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Kwa hiyo, ripoti ya suala hilo italetwa kwenye Bunge la Septemba au lile la Novemba kwa hatua zaidi,” alisema.
BAADHI YA WABUNGE HAWANA VIWANGO
Akizungumzia eneo hilo, alisema baadhi ya wabunge hawana viwango vinavyotakiwa ingawa wamechaguliwa na wananchi.
“Kanuni zinamchukulia mbunge ni mtu mzima, wa hadhi fulani na mstaarabu fulani ambaye ni kiongozi.
“Lakini, kadiri uchaguzi unavyozidi kwenda, wengine wanatoka vyuo na ni watu wa aina aina kutoka mitaani, lakini wamechaguliwa ingawa wengine wako chini ya viwango vilivyotarajiwa.
BUNGE LIVE
Akizungumzia kitendo cha matangazo ya Bunge ya moja kwa moja kusitishwa, alisema uamuzi huo ni sahihi na kwamba umewasaidia kwa kiwango kikubwa.
“Kwa sasa ni uamuzi sahihi, lakini hakuna uamuzi ambao hauwezi kurekebishwa kwa sababu baadhi ya wabunge wanapojua wanaonekana Live, wanafanya usanii bungeni,” alisema.
“Kwa mfano, wakati ule mbunge anaweza akawaambia watu wake, kuwa leo nafanya vurugu, hivyo mniangalie,”alisema.