27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai amshukia Zitto, naye ajibiwa

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

SIKU chache baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuiandikia barua Benki ya Dunia (WB), kuitaka kusitisha kuikopesha Tanzania Dola za Kimarekani milioni 500 za kuendeleza elimu, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wanamsubiri ili awaeleze lengo lake lilikuwa ni nini.

Katika barua yake aliyoiandikia WB Januari 22 mwaka huu, huku akitumia nembo ya Bunge la Tanzania, Zitto aliitaka benki hiyo kuahirisha mkopo huo kabla mabadiliko ya kisera kuhusu elimu kufanyika.

Jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni, Spika Ndugai alieleza kushangazwa kwa mwenendo wa baadhi ya wabunge huku akimtolea mfano Zitto kwa kuiandikia barua WB ili nchi ikose fursa ya mkopo ambao lengo lake ni kuboresha elimu.

“Wakati mwingine waheshimiwa mwenendo wetu hauweleweki, mfano mbunge mwenzetu akirudi labda atatufafanulia, mheshimiwa Zitto kuandika barua WB kwamba nchi yetu ikose fursa ya mkopo ambao lengo lake ni elimu kwa sababu ya tofauti za kisera ambayo ni jambo la kawaida.

“Mtu unaweza kuwa na tofauti za sera au mtazamo kati ya wewe mbunge na Serikali na kadhalika, lakini kufikia mahali kublock  (kuzuia) Tanzania isipate fursa fulani nadhani ni kwenda mbali mno kwa sababu watoto watakaokosa fursa hiyo ni watoto wa Tanzania, walimu wa Tanzania, miundombinu ya elimu ya Tanzania.

“Na sijui katika hilo kama mbunge unafaidika nini, kwa sababu kama ni tofauti za kisera haya mambo ni ya kujadili tu na ndio maana sisi ni wabunge tupo  hapa, kwa kweli limetugusa na kutukera wengi ambao bado hatujaelewa linakujakujaje?

“Ningependa kutoa ushauri kwamba ni vyema kutumia fursa zetu kama wawakilishi wa wananchi tukaelimishana na kuelezana kuliko kuwakosesha Watanzania fursa wakati baadhi yetu hapa watoto wetu wako Feza Boys na Marian Girls halafu unablock msaada kwa watoto walio wengi ambao ni wa wapigakura wetu jambo ambalo nadhani halifai kabisa,”alisema Ndugai.

Kutokana na hilo, muda mfupi baadaye Zitto alimjibu Ndugai kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, akisema hakuna tofauti ya kisera katika suala la watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo.

“Kwa spika Ndugai; hakuna tofauti ya kisera katika suala la watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo, ilani ya CCM iliahidi hilo kwa wananchi mwaka 2015, vyama vya upinzani viliahidi hili na wananchi wanaunga mkono hili,”aliandika Zitto ambaye yuko nje ya nchi.

Juzi akihojiwa na BBC Dira ya Dunia, Zitto alisema, “Ni dhahiri kuwa mkopo wa Benki ya Dunia kwa ajili ya elimu Tanzania utanufaisha watu wengi sana, lakini ukitekelezwa kwa namna ulivyopangwa hivi sasa utabagua pia watoto wengi sana. Na hoja yetu ya msingi ni kuboresha, hoja yetu si kuzuia mkopo.

“Kwa namna ambavyo mkopo umetengenezwa maana yake ni kwamba watoto wa kike wa Tanzania ambao watapata ujauzito njia yao mbadala ya kupita itakuwa ni kwenda kuwa wapishi, wasafishaji, wafumaji, washonaji na hatuwezi kwenda kutengeneza taifa la kuwafanya watoto wa kike kwa sababu tu ya kupata ujauzito asiweze kuwa na chaguo katika elimu.”alisema Zitto.

Juzi, Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbas aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa mkopo huo haujasitishwa bali majadiliano yanaendelea.

Katika hilo, aliwatoa hofu Watanzania kuhusu madai kuwa WB imesitisha kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 500 kwa Tanzania, akibainisha kuwa bado wapo kwenye mazungumzo.

Vilevile alijibu madai ya Zitto kwamba Tanzania imenyimwa mkopo huo kwa madai kuwa fedha hizo zitatumika katika uchaguzi mkuu badala ya elimu.

“Tulifanya uchaguzi wa Serikali za mitaa, chaguzi za marudio na sasa tume za uchaguzi zinafanya vikao kwa ajili ya uchaguzi, sasa fedha hizo zinatoka Benki ya Dunia? Dunia haiwezi kuamini maeneo yake (Zitto). Dunia ina akili, ina macho,”alisema Dk. Abbas.

Dk. Abbas alieleza hayo baada ya kikao cha bodi ya utendaji ya Benki ya Dunia ambacho kingetoa uamuzi kuhusu kuruhusu mkopo huo kuripotiwa kuahirishwa.

Kikao hicho kilipangwa kufanyika Januari 28 mwaka huu 2020 kwa ajili ya kuidhinisha mkopo huo, lakini kikaahirishwa dakika za mwisho kutokana na kile kilichoripotiwa na vyombo vya habari vya nje kuwa ni ombi la taasisi ya kijamii ambayo ina wanachama wake Tanzania.

Kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho, mkurugenzi anayehusika na haki za watoto wa taasisi ya kimataifa inayojishughulisha na haki za binadamu ya Human Rights Watch (HRW), Zama Neff aliiomba WB kuchelewesha fedha hizo hadi suala la wasichana wanaopata mimba shuleni litakapopatiwa ufumbuzi kuhusu mustakabali wa elimu yao.

Zitto aliiandikia barua WB akiomba ihahirishe mkopo huo kwa kuwa mwenendo wa hapa nchini umekuwa mbaya kwa kuwepo uvunjifu wa haki za binadamu, vyama vya upinzani haviruhusiwi kufanya mikutano ya kisiasa.

“Wiki iliyopita tu polisi walizuia mimi kufanya mkutano wa hadhara na wapiga kura wangu, pia wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba mwaka jana vyama vya upinzani hatukuruhiswa kufanya mikutano isipokuwa CCM tu.

“Pia mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu kwa nchi yetu hivyo ni wazi fedha hizo zinaweza kwenda kutumika kwa ajili ya uchaguzi, hivyo naomba mkopo huo uharishwe mpaka hapo marekebisho yatakapofanya ili mkopo uendelee.”

Wengine waliowahi kuingia kwenye 18 za Ndugai

Zitto anakuwa mbunge wa tatu kuingia kwenye 18 za Spika Ndugai baada ya aliyekuwa Mbunge wa Singira Mashariki, Tundu Lissu, na Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele  (CCM).

Lissu ambaye baadaye Ndugai alitangaza  kumvua ubunge kutokana na alichosema ni kushindwa kuudhuria mikutano mitatu mfululizo bila kuwa na ruhusa ya Spika, aliingia kwenye 18 za Ndugai baada ya kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya kimataifa akieleza  alivyopigwa risasi akiwa kwenye shughuli za bunge pamoja na kutotibiwa na Serikali na kunyimwa baadhi ya stahiki zake za Bunge.

Kutokana na hali hiyo, Ndugai alieleza kumshangaa kwake Lissu huku akisema anashangaa ni vipi ametoka ubeligiji alipokuwa akitibiwa na kwenda Uingereza, Ujerumamani, Marekani na kuongea na vyombo vya habari huku akishindwa kumuandikia Spika kujua hali yake na kuomba ruhusa.

Kwa Upande wa Masela ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Africa (PAP), aliingia kwenye mgogoro na Ndugai baada ya kumtaka kurudi nchini ambako pia atafikia mikononi mwa Kamati za Maadili za Bunge na chama chake (CCM).

 Spika Ndugai alisema mbunge huyo amekuwa akifanya mambo ya hovyo na kugonganisha mihimili.

“Amefanya mambo ya utovu wa nidhamu huko  na taarifa tumezipata na hata kwenye mitandao imeonekana, sasa tumemtaka arudi lakini amegoma hivyo nimemwandikia barua Rais wa PAP kusimamisha kwa muda ubunge wa mheshimiwa huyu had I tutakapotoa taarifa nyingine,” alisema Ndugai.

Baada ya Masele kuwasili nchini na kuhojiwa na kamati husika, alipata fursa ya kuzungumza bungeni na ambapo pamoja na mambo mengine alisema “nilitafakari sana maslahi ya wabunge, taifa na kijana ninayekua. Nilifikilia haraka kama Spika ananisimamisha bila kunisikiliza ndio sababu ya kukata rufaa kuwasiliana na viongozi wa CCM na Waziri Mkuu.”

Ninasikitika kwamba sikuchonganisha mihimili, nisingeweza kupeleka jambo hili kwa waziri,” alisema huku akionyesha barua hiyo.

Akizungumzia video iliyosambaa mitandaoni ikimuonyesha akizungumza katika Bunge hilo lililokuwa likiendelea Afrika Kusini na kumalizika Mei 17 mwaka jana, Masele alisema Rais wa bunge hilo alitaka kumng’oa katika madaraka kwa kutumia barua aliyotumiwa na Ndugai.

Baada ya Masele kumaliza kuzungumza, Ndugai alisema, walimuita Masele nyumbani (Tanzania) kwa kuwa aliwaandikia viongozi wa juu ujumbe wa ajabu, “akigonganisha mihimili na ndio sababu tulimtaka arudi lakini alikaidi.

“Tatizo lako ni uongo, kugonganisha viongozi, fitina na uchonganishi. Binafsi nimesononeka sana na naendelea kusononeka. Hata wewe huelewi.

“Ameniambia aombe radhi halafu anasema mengine. Hatujakuita kwa hayo ya PAP, tumekuita kwa haya ya nyumbani. Acha tabia hizo, acha, ujanja ujanja wa kuzungusha maneno.”

Baada ya maelezo hayo, Ndugai aliliomba Bunge kumpuuza Masele hoja iliyoungwa mkono na wabunge waliosimama na kushangilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles