MOSCOW, URUSI
NDEGE ya Jeshi la Urusi iliyokuwa na watu 92 wakiwamo waimbaji, wanenguaji na wanamuziki wengine wa Jeshi la Urusi ilianguka katika Bahari Nyeusi wakati ikielekea Syria jana na kuwaua watu wote hao.
Kwa mujibu wa maofisa wa Urusi, wanamuziki hao walitarajia kufanya tamasha ya mwaka mpya katika kambi ya Urusi mjini Latakia, Syria.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, ndege hiyo aina ya TU-154 Tupolev ilitoweka kutoka rada alfajiri ya jana, dakika mbili tu baada ya kuruka kutoka Sochi, kusini mwa Urusi, ambako ilisimama kwa muda kujaza mafuta ikitokea Moscow njiani kuelekea Syria.
Msemaji wa wizara hiyo, Meja Jenerali Igor Konashenkov, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo.
Eneo la ajali limeshabainishwa na tayari meli, helikopta na ndege zisizotumia na rubani zimeanzisha uchunguzi huku mabaki yakiripotiwa kupatikana kilomita moja na nusu kutoka pwani.
Aidha chanzo kimoja cha habari kilisema ndege hiyo haikuwa imetuma tahadhari na hapakuwa na ishara ya kuwepo matatizo, na rubani alikuwa ametulia hadi ndege hiyo inatoweka.
Katika taarifa yake kwa njia ya televisheni, akiwa mji wake wa nyumbani wa St. Petersburg, Rais wa Urusi Vladimir Putin ametangaza leo kuwa ni siku ya kitaifa ya maombolezo.
Ndege hiyo iliyotengenezwa mwaka 1983 wakati wa zama za Muungano wa Kisovieti, ilikuwa imebeba abiria 84 na wafanyakazi wanane.