KHARTOUM, SUDAN
WAKUU wa Sudan wametangaza habari ya kutunguliwa ndege moja isiyo na rubani (droni) juu ya anga ya makazi ya Mkuu wa Baraza la Uongozi la nchi hiyo, Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan.
Kikosi maalumu cha kumlinda Luteni Jenerali al Burhan kimetangaza kuwa, droni moja iliyokuwa inaruka karibu na makazi ya mkuu huyo wa Baraza la Uongozi imetunguliwa mjini Khartoum.
Baada ya tukio hilo imebainika kwamba ndege hiyo isiyo na rubani ilikuwa ni ya Jeshi la Polisi la Sudan na ilikuwa imetumwa kuchunguza ni kiasi gani wananchi wametii amri ya kutotoka nje mjini humo kama njia ya kupambana na maambukizi ya kirusi hatari cha corona.
Aidha duru za usalama za Sudan zilisema kuwa, kikosi maalumu cha kumlinda Burhan hakikuwa kimepewa taarifa kuhusu operesheni ya droni hiyo.
Viongozi wa Sudan wametangaza karantini na amri ya kutotoka nje katika miji yote ya nchi hiyo kama njia ya kukabiliana na maambukizi ya corona.
Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa mwezi huu Machi, Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok alisalimika kuuawa katika jaribio lililofeli mjini Khartoum.
Sudan ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kabisa kuripoti maambukizi ya kirusi cha corona barani Afrika.
Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Waziri wa Habari wa Sudan, Faisal Saleh alisema kuwa raia wawili wa nchi hiyo waliorejea nyumbani kutokea China walikuwa wanashukiwa kuwa wamepatwa na kirusi cha corona.
Mwezi uliofuata wa Februari, timu ya madaktari 35 wa Kichina walitumwa nchini Sudan kutoa mafunzo juu ya jinsi ya kuepuka maambukizi ya kirusi hatari vya corona na njia za kupunguza makali ya ugonjwa wa Covid-19.