NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NDEGE mpya ya kwanza iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam jana, ikitokea Canada ilikotengenezwa.
Ndege hiyo aina ya Bombadier Q400 NextGen ilitua saa 6.00 mchana na kisha kupatiwa heshima maalum ambayo hutolewa kwa ndege yoyote mpya inayotua katika nchi husika (Water Salute).
Baada ya kupokea heshima hiyo, ndege hiyo iliegeshwa katika eneo la ndege za jeshi Ukonga (Airwing Ukonga).
Akizungumza baada ya kuwasili
ndege hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamriho alisema ndege ya pili itawasili baada ya wiki moja.
“Baada ya kuwasili ndege ya pili ndipo yatafanyika mapokezi rasmi yatakayoongozwa na Rais John Magufuli kwa tarehe itakayotangazwa baadaye,”alisema Dk. Chamriho.
Mkataba wa makubaliano ya awali ya ununuzi wa ndege hizo ulitiwa saini Dar es Salaam, Agosti, 2014 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro na Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni hiyo ya Bombardier Kanda ya Afrika.
Bombardier ni kampuni pekee duniani inayotengeneza ndege na treni za kisasa kwa pamoja. Makao makuu ya kampuni hiyo yako Montréal, Canada.
ATCL lilianzishwa Machi 11,1977 baada ya kuvunjika kwa lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki. Kwa sasa shirika hilo lina ndege moja tu ya Dash 8, Q300.