Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Shirika la Taifa la Maendeleo(NDC ), limesema linaandaa sheria mpya ambayo itazingatia hali halisi ya mfumo wa uendeshaji uchumi nchini na kufanya shirika kuwa chombo mahususi cha serikali cha kuchochea mabadiliko ya mfumo wa uchumi, biashara, kusaidia maendeleo na kuwezesha uwekezaji.
Akizungumza leo Septemba 26,2023, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya Shirika hilo kwa mwaka wa fedha 2023/24, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dk. Nicolaus Shombe amesema wamekuwa na mchango mkubwa kimapato, ajira katika pato la taifa.
“Sheria mpya na mfumo wa uendeshaji wa shirika unaopendekezwa utazingaita haja ya kuweka mifumo rahisi wa kufikia maamuzi kuliwezesha shirika kushirikiana na sekta binafsi na kutumia fursa za kibiashara zinazojitokeza,”amesema Dk.Shombe.
Amesema mpango mkakati wa shirika umehusisha na umeainisha maeneo ya mikakati ambayo shirika linawekeza kwa kushirikiana na wawekezaji mahiri wa ndani na nje ya nchi lengo ni kuifanya NDC ambalo lina nafasi kuchangia ujenzi wa Taifa.
“Kuna maeneo muhimu ambayo sekta binafsi inasita kuwekeza au inashindwa kuwekeza kutokana na sababu uwezo wa mitaji na Teknolojia muda mrefu kupata manufaa na sababu nyingine za kibiashara shirika linaweza kuwekeza ili kuvutia wawekezaji wengine, “amesema.
Aidha amesema shirika hilo limeweza kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo mradi wa Liganga na Mchuchuma uliopo Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe kubaini uwepo wa mashapo ya chuma kias cha tani milioni 126 eneo kilomita za mraba 10 na makaa ya mawe tani milioni 426 kwenye eneo kilomita za mraba 30.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajia kuchimba chuma tani milioni 2.9 kwa mwaka na kuzalisha bidhaa za chuma tani milioni moja kwa mwaka.
“Shirika limefikiwa kulipa fidia ya jumla shilingi bilioni 15.4 kwa wananchi wanaoishi mahali mradi unapotekelezwa wa miradi ya Mchuchuma shilingi bilioni 5 na Liganga shilingi bilioni 10 ambazo zimetolewa na serikali hadi kufikia Juni 30, mwaka huu na jumla ya wanufaika 1048 wamelipwa kati ya 1142,”amesema.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa leseni za wachimbaji wadogo wa makaa ya mawe unaruhusu shirika kuanza uchimbaji huo ambapo kampuni tano za wazawa zinatarajia kuanza uchimbaji katika eneo la Mchuchuma ndani ya mwaka 2023/24.
Dk.Shombe amesema shirika limeendelea na mikakati mbalimbali ya kukifufua na kuboresha kiwanda cha mikakati cha KMTC kilichopo Hai katika Mkoa wa Kilimanjaro.