PATRICIA KIMELEMETA
WAKUU wa shule za serikali na binafsi wametakiwa kuhakikisha maeneo yanayozunguka shule zao hayageuki kuwa vijiwe vya wavuta bangi na wauza dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema maeneo ya shule yenye viwanja vya michezo yamekuwa yakigeuzwa vijiwe vya wavutaji na watumiaji wa dawa za kulevya jambo ambalo lina athari mbaya kwa wanafunzi.
Alisema, walimu wanapaswa kuwasimamia walinzi wa shule waimarishe ulinzi ili maeneo ya shule yasigeuke vijiwe vya mihadarati.
“Kuna baadhi ya shule zinahatarisha mienendo ya wanafunzi katika masomo kwa kuwepo baadhi ya vijana wanaoyageuza vijiwe vya kuvuta bangi na kutumia dawa za kulevya.
“Walimu wakuu na wamiliki wa shule wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika shule zao ili kuondoa vijana hao kwa sababu wanaweza kuwashawishi wanafunzi kushiriki katika utumiaji wa dawa hizo, alisema Waziri Prof. Ndalichako.
Alisema idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya ni vijana walio masomoni na wanaoishi nyumbani bila kazi hivyo walimu wanapaswa kuzungumza nao ili wasijiunga kwenye utumiaji wa dawa hizo.
“Kuna baadhi ya wazazi wanashindwa kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao jambo linalochangia kuongezeka kwa utumiaji wa dawa za kulevya kwa wanafunzi. Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake,”alisema Waziri Prof. Ndalichako.