– DAR ES SALAAM
SEKTA ya afya nchini imetetereka, kutokana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuwa na akiba ya makopo 173 ya vidonge vya Panadol kwa nchi nzima.
Mbali na hilo vifaa vya kujifungulia wanawake wajawazito navyo vimekosekana kwa miezi miwili mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, hali hiyo imetokana na Serikali kushindwa kupeleka fedha za bajeti ya dawa MSD kwa wakati.
Pamoja na hali hiyo dawa ambazo zimekuwa zikitumika sana Ciprofloxacin, Cetriaxone, Panadol, Diclofenac, Trimoxazol, Amoxycline, Doxycline na Metronidazol ambazo upatikanaji wake umekuwa wa kusuasua.
Taarifa iliyotolewa na MSD katika tofauti yake na uchunguzi uliofanywa zinaeleza kuwa kwa kupindi cha miezi mitatu mfululizo, kumekuwa na mtikisiko huo unaohatarisha afya za Watanzania kutokana na kukosekana dawa muhimu ikiwemo za maumivu.
MSD ambao ndiyo wasambazaji wakuu wa dawa na vifaa tiba nchini, imejikuta ikikumbwa na uhaba mkubwa kutokana na kuporomoka kwa mtaji wake na kupewa bajeti isiyojitosheleza.
Ingawa, serikali imeongeza fedha kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba kwa kiwango kikubwa kufikia Sh bilioni 250 kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 ikilinganishwa na Sh bilioni 29.2 zilizotengwa mwaka wa fedha uliopita 2015/16,
Kutokana na hali hiyo Serikali ilipaswa kuipa MSD Sh bilioni 62.5 katika kipindi cha Julai hadi Septemba lakini imepatiwa Sh bilioni 20 tu ambapo ni sawa na asilimia 32 pekee katika kipindi hicho.
Taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya MSD inaonesha tangu Machi hadi Septemba mwaka huu, mwenendo wa dawa muhimu umekuwa kati ya sifuri na kwa viwango ambavyo havitoshelezi mahitaji.
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la SIKIKA, Irenei Kiria, ambaye alisema kuwa hali ya ukosefu wa dawa nchini inasikitisha.
Alisema hata katika utafiti wao walioufanya hivi karibuni ilibainika uwepo wa makopo 173 ya dawa za maumivu (Panadol).
“Idadi hii ni sawa na kutokuwa nazo maana dawa hizi zinaweza zisitoshe hata hospitali moja hasa kwa kuzingatia mfumo wa uingizaji uliopo,” alisema.
Kiria alisema hali duni ya upatikanaji imeonekana hata kwa dawa zinazotumika mara kwa mara katika kuhudumia makundi maalumu.
“Kwa mfano sindano ya Oxytoxin na Delivery Kits ambazo zinahitajika wakati wa kujifungua, dawa za Antibiotics, magonjwa ya moyo na kuharisha hazipo kabisa,” alisema.
Alisema licha ya kuwapo kwa uhitaji mkubwa lakini bajeti zinazotengwa kila mwaka kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba hazijawahi kulingana na mahitaji halisi.
“pamoja na kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezungumzia juu ya maendeleo ya utekelezwaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,
“Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya uliopita (HSSP) III na wa sasa HSSP IV imetambua kuwapo kwa changamoto ya upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba nchini. HSSP imebainisha changamoto zinazoikabili MSD ni kuporomoka kwa mtaji, bajeti isiyojitosheleza na upatikanaji mdogo wa dawa,” alisema Kiria.
Pamoja na hali hiyo alisema ripoti ya ukaguzi wa MSD iliyofanywa na Global Fund (mfuko wa dunia) kwa mwaka jana imeonesha kuwa na ongezeko la dawa na vifaa tiba vya misaada kwa Serikali hivyo kuilazimu MSD kutumia mtaji wake kugomboa misaada hiyo.
“Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kumaliza mtaji wa MSD, bajeti ni ndogo ya fedha pamoja na kupungua kwa mtaji vimeipelekea MSD kununua bidhaa chache kuliko mahitaji ya nchi na hii inajidhihirisha kwa kuangalia viwango vya sasa vya dawa muhimu na vifaa tiba vilivyopo MSD.
“Bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba imeongezeka hadi Sh bilioni 250 toka Sh bilioni 29.2 mwaka 2015/16 huku MSD, imepewa Shilingi bilioni 20 tu.
“Swali la kujiuliza, je kiwango hiki kitaweza kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa muda mfupi? Ukizingatia kuwa mchakato wa ununuzi unachukua si chini ya miezi tisa tangu uanzishwaji wa zabuni mpaka uwasilishwaji bidhaa?,” alisema na kuhoji
Alisema pamoja na mipango mbalimbali ya Serikali katika bajeti ya 2016/17 iliyowasilishwa bungeni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha Ofisi za Kanda za MSD, ili kuongeza upatikanaji wa dawa kwa vituo vya kutolea huduma, mojawapo ya mikakati aliyoeleza ni kuhakikisha MSD inanunua dawa moja kwa moja viwandani kupunguza gharama zinazotokana na kutumia wachuuzi binafsi,” alisema.
Alisema ni miezi mitatu imepita tangu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha lakini hali bado hairidhishi katika maghala ya MSD licha ya kuwapo kwa mikakati hiyo.
“Swali la kujiuliza ni kwa nini hatuoi mabadiliko katika MSD miaka yote hii? Mipango na mikakati iliyopo inafanyiwa kazi kwa vitendo? Je ni wakati mwafaka kwa MSD kufanya kazi kwa kujitegemea ili kushindana na soko binafsi,” alihoji.
Alisema kutokana na upungufu huo uliopo MSD, hivi sasa baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya vinalazimika kununua mahitaji kutoka kwa wachuuzi binafsi.
Kauli ya Waziri
MTANZANIA lilimtafuta Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ili kupata kauli ya Serikali juu ya hali hiyo.
Alisema ni kweli kujitosheleza kwa bajeti ya dawa kwa asilimia 100 ni changamoto lakini jitihada kubwa zimefanyika na zinaendelea kufanywa na serikali.
“Muhimu kwetu ni kusimamia mapato na matumizi za pesa katika ngazi zote ya MSD, hospitali za rufaa za mikoa, wilaya na vituo. Pia tumeamua kununua dawa kutoka kwa wazalishaji badala ya wafanyabiashara. Dawa sasa zitapatikana nyingi na kwa bei nafuu,” alisema.
KAULI YA MSD
Kufuatia hali hiyo, MTANZANIA lilimtafuta, Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu, ambaye alisema hali hiyo ilichangiwa na mchakato waliokuwa wakiutumia zamani kuagiza dawa mbalimbali.
“Ni kweli tunaidai Serikali, lakini deni hilo limeshaanza kulipwa, zamani tulikuwa tunaagiza dawa kutoka kwa wasambazaji jambo ambalo lilikuwa linatulazimu kila mara kufanya mchakato wa tender (zabuni) hatua ambayo ilikuwa inachukua muda mrefu.
“Lakini sasa hivi tumeanza kuagiza dawa moja kwa moja toka viwandani, tumeingia mkataba wa muda mrefu wa manunuzi (Frame work contractor) na nchi ya Thailand, Kenya, Uganda na India ambapo tutakuwa tukinunua dawa muda wowote tutakaokuwa tukihitaji,” alisema.
Alisema kupitia mkataba huo watanunua dawa zaidi ya 30 na kwamba kwa kuanzia wameagiza dawa 14 na kati ya hizo tisa zimeshawasili nchini ambazo ni zile za kutuliza maumivu na antibiotics.
“Tumepewa hizo Sh bilioni 20 ikiwa ni robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, fedha nyingine tutapewa ifikapo Novemba 11, mwaka huu ambayo itakuwa robo ya pili ya mwaka, hizo Sh bilioni 20 ndizo ambazo tumezitumia kuagiza dawa hizo, zimeletwa tisa nyingine tano tunatarajia kuzipokea Oktoba, mwaka huu,” alisema.
Alisema MSD imeshaanza kusambaza dawa hizo katika kanda zake ili ziweze kuwafikia wananchi kwa kusambazwa katika hospitali zote nchini.
“Dawa tisa zilizowasili kati ya 14 zilizoagizwa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ni Ciprofloxacin, ceftriaxone, Paracetamol, diclofenac, co-trimoxazol, amoxycline, doxycycline, metronidazol ambazo zote ni dawa muhimu zaidi kwa magonjwa ya binadamu,” alizitaja.