Mwandishi Wetu, Arusha
Wataalamu 25 wa Ulinzi na Usalama wa vyanzo vya mionzi kutoka nchi sita za Afrika, wanashiriki katika mafunzo ya wiki mbili ya utoaji mafunzo ya ulinzi na usalama wa vyanzo vya mionzi yanaoendeshwa na Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Peter Ngamilo, amesema mafunzo hayo yanayofanyika jijini Arusha yana lengo la kuwapatia ujuzi wakufunzi hao namna ya kufundisha wataalamu mbali mbali wanaohusika na usalama wa vyanzo vya mionzi katika nchi zao.
“Baada ya mafunzo hayo, wakufunzi hao watakuwa na uwezo wa kuchukua nafasi ya kuongoza katika mafunzo kwa wafanyakazi wa kitaifa katika nchi zao katika kuhakikisha kuwa vyanzo vya mionzi vinatumika katika njia zilizo salama na halali.
“Vyanzo vya mionzi visipodhibitiwa vinaweza kutumika na katika vitendo vya kigaidi na kuleta madhara makubwa kwa jamii na kuathiri shughuli za maendeleo na uchumi,” amesema.
Pamoja na mambo mengine pia amesema washiriki watapata fursa ya kufundishwa na kubaini usafirishaji haramu wa vyanzo vya mionzi hasa kwa wataalamu wa mamlaka za ulinzi na usalama ikiwamo Polisi, Walinzi waliopo mipakani na wasimamizi wa teknolojia ya nyuklia, maofisa wa forodha na wataalamu wa kupambana na majanga ya nyuklia.
Pia, Ngamilo ametaja nchi wanazotoka washiriki hao kuwa ni Burundi, Uganda, Congo (DRC), Zambia, Ghana na wenyeji Tanzania.