25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NBC hatarini kufilisiwa

NBCNA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), ipo hatarini kufilisiwa kutokana na kushindwa kulipa deni la Sh bilioni 22.4 inazodaiwa na kundi la kibenki la Afrika Kusini la ABSA Group Limited.

ABSA kwa sasa inamiliki asilimia 55 ya hisa za benki hiyo na Serikali ikibakiwa na asilimia 30, huku asilimia nyingine 15 za hisa zikimilikiwa na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) kutoka World Bank Group.

Akizungumza jana katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Ofisa Msajili Hazina, Domi Malosha, alisema kuwa deni hilo limetokana na hasara iliyopatikana mwaka 2010 hadi 2012 baada ya mtaji wa biashara kushuka kwa asilimia 12 na kusababisha kushindwa kujiendesha.

Alisema mtaji huo ulishuka baada ya kupata hasara ya kukopesha magari yanayodaiwa kuwa mabovu yenye thamani ya Sh bilioni 50, hali iliyosababisha Benki Kuu (BoT) kubaini chanzo cha tatizo.

Malosha alisema ili kujinasua, Serikali na wanahisa wa benki hiyo walimtafuta mkaguzi kufanya utafiti wa chanzo cha hasara hiyo ambaye kabla ya kumaliza kazi hiyo alikimbia bila ya kuwasilisha ripoti.

Alisema BoT iliwataka wanahisa kutafuta mtaji wa uwekezaji wenye thamani ya Sh bilioni 75.

“Kila mwanahisa alitakiwa kulipa kulingana na hisa zake, kutokana na hali hiyo, ABSA ilitakiwa kulipa sh bilioni 25, IFC ilitakiwa kulipa bilioni 25 na Serikali ilitakiwa kulipa kiasi cha shilingi bilioni 22.4,” alisema Malosha.

Aliongeza kutokana na hali hiyo Serikali ikashindwa kulipa kiasi hicho hali iliyosababisha Serikali kukopa fedha hizo kwa ABSA ili  iweze kulipa deni hilo.

“Mkabata wa deni hilo ulitoa masharti ya kuwalipa ABSA ndani ya miaka miwili ambayo inamalizika Machi 31 mwakani, hadi sasa Serikali imeshindwa kulipa kiasi hicho hivyo kusababisha hisa za Serikali kuwa shakani kutaifishwa,” alisema.

Malosha alisema kuwa katika kuhakikisha wanampata aliyesababisha hasara, Serikali ilitafuta mkaguzi mwingine ili aweze kufanya ukaguzi upya ambaye hadi sasa bado anaendelea na kazi hiyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe aliuliza sababu za kutumia mkaguzi wa nje kufanya kazi hiyo badala ya wakaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akijibu Malosha alisema Serikali haitakubaliana na ripoti itakayotolewa na mkaguzi huyo, mkataba unawaruhusu kutafuta mkaguzi mwingine ili aweze kufanya kazi hiyo.

Zitto alisema kamati hiyo imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kupitia upya mikataba yote ya Serikali na ABSA katika benki ya NBC.

Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Filikunjombe, alisema kamati hiyo itahakikisha inalinda maslahi ya wananchi na hakutatokea ufisadi kama ulivyotokea kwenye Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel.

“Hawa watendaji wanaingia mikataba mibovu hali inayosababisha hisa za Serikali kumilikiwa na makampuni ya nje, tutahakikisha maslahi ya wananchi yanalindwa,” alisema Filikunjombe.

Hata hivyo, ABSA imekwishauzwa na kununuliwa na Benki ya Kimataifa ya Barclays na taarifa nyingine mpya zikibainisha kuwa mmoja kati ya wamiliki watatu wa NBC, yaani IFC, ipo tayari kuuza hisa zake.

Hadi kufikia Desemba mwaka 2010, NBC ilikuwa na mali zenye thamani ya Sh trilioni 1.47, amana za wanahisa kiasi cha Sh. bilioni 153.1, hiyo ni kwa mujibu wa tovuti ya benki hiyo.

NBC ilianzishwa mwaka 1967 wakati Serikali chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilipofanya utaifishaji wa taasisi za fedha, zikiwamo benki.

Mwaka 1997, NBC iligawanywa katika taasisi tatu ambazo ni NBC Holding Corporation, National Microfinance Bank (NMB) na NBC (1997) Limited.

Baada ya mgawanyo huo, mwaka 2000 ABSA ilinunua hisa nyingi za NBC (1997) Limited, ununuzi ambao ulizua upinzani mkali nchini ikielezwa kuwa ni uuzaji wa bei ya kutupwa.

Uuzaji huo ulipingwa vikali na Mwalimu Nyerere ambaye kwa ujumla hakuwa akifurahishwa na mchakato wa ubinafsishaji na hasa unaohusu mashirika ya umma yaliyokuwa yakijiendesha kwa faida.

Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Shabani Matutu na Grace Shitundu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles