26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

NASA WATAKA RAILA ATANGAZWE MSHINDI

NAIROBI, KENYA

WAKATI Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikiwa imedokeza itatangaza baadaye leo mshindi wa urais, muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), umeitaka imtangaze mgombea wake kuwa mshindi wa kiti hicho.

Tamko la NASA ni mwendelezo wa kupinga matokeo yanayotangazwa na tume hiyo mtandaoni, yakionyesha Rais Uhuru Kenyatta anaongoza dhidi ya mgombea wake, Raila Odinga.

Viongozi wa NASA wamesema walikutana na wakuu wa IEBC na kuwasilisha rasmi malalamiko yao kupitia barua.

Wakala mkuu wa NASA, Musalia Mudavadi, ambaye ni naibu waziri mkuu wa zamani, alisema upinzani umepata maelezo zaidi kuwa matokeo ya uchaguzi yalivurugwa baada ya kudukuliwa kwa mitambo ya IEBC.

Hata hivyo, makamishina wa IEBC wamekanusha kuwa mitambo ilidukuliwa na Mwenyekiti Wafula Chebukati amesema kulikuwa na jaribio la kuidukua, lakini halikufanikiwa.

Mudavadi alisema IEBC inapaswa kutoa mwelekeo kamili kwa vile ukweli unaonyesha Raila ndiye aliyeibuka mshindi.

“Tumepata habari kutoka kwa wanaotujuza IEBC, kuwa Raila amepata kura 8,041,726 huku Uhuru akipata kura 7,755,428, lakini matokeo haya yamebadilishwa kusomeka Uhuru akiongoza kwa kura 8,056,855, Raila kura 6,659,493,” alidai Mudavadi wakati akizungumza na wanahabari jana jioni jijini Nairobi.

Hata hivyo, kinara huyo ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha ANC – mshirika katika NASA, amekataa kuwafichua waliowapa taarifa hizo, kwa kile alichosema kuhifadhi majina yao.

“Kama mlivyoona kile Chris Msando alichofanyiwa, hatutafichua majina ya waliotujuza kwa usalama wao,” alisema.

Msando alikuwa kaimu meneja wa mawasiliano IEBC kabla ya kuuawa katika hali ya kutatanisha wiki moja iliyopita.

“Mahakama ikiagiza tuwafichue, mawakili wetu watakabiliana na swala hili,” alieleza Mudavadi.

Matokeo ya kura yanayoendelea kuhesabiwa na kutolewa na IEBC kutoka kwenye kituo kikuu cha kujumuisha kura cha Bomas of Kenya jijini Nairobi, yanaonyesha Rais Uhuru wa Jubilee anaongoza kwa kura 8,114,291 huku kinara wa NASA, Raila akizoa kura 6,716,552.

Muungano wa NASA aidha unataka IEBC isitishe kurusha matangazo ya matokeo hayo. “Tunataka watangaze Mheshimiwa Raila Amollo Odinga kuwa Rais na Kalonzo Musyoka Naibu wake,” alisema Mudavadi.

Kiongozi huyo alifichua kuwa Raila atazungumza baada ya IEBC kutangaza rasmi matokeo.

Aidha Mudavadi amekanusha kuwa msimamo wao utachochea ghasia kwa Wakenya.

“Hatuzui ghasia zozote, wala hatufanyi kazi ya IEBC, lakini matokeo wanayopeperusha si halali,” alisisitiza huku akiwaomba Wakenya kubakia watulivu.

“Utendaji kazi wa IEBC unasalia kwao, tutapeana mwelekeo wetu baada ya matangazo kutolewa,” aliongeza.

Nchini Kenya, ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutangaza matokeo au kusambaza matokeo ambayo hayajatoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Ni tume hiyo ya uchaguzi pekee inayoruhusiwa kutangaza matokeo.

Kuhusu kauli za waangalizi wa kimataifa kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, Mudavadi alisema wanakubaliana nao ila hawafahamu kilichojiri.

“Ni rahisi kwao kusema uchaguzi ulikuwa wa huru, haki na wazi, lakini hawajui kilichotokea,” ameeleza Mudavadi aliyekuwa ameandamana na Raila, mkewe  Ida Odinga, mgombea mwenza Kalonzo Musyoka, Seneta wa Siaya, James Orengo na viongozi wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles