ADAM MKWEPU NA MITANDAO
Mesut Ozil kuendelea kuwapo katika kikosi cha Arsenal msimu ujao ni kama ndoto.
Safari ya kuondoka viunga vya Londoni ya Kaskazini imewadia kwa kiungo huyo mahiri ambaye ni muhanga wa ujio wa Unai Emery pale Arsenal tangu Arsene Wenger aondoke baada ya kuiongoza timu hiyo kwa miaka 22.
Tangu Emery atue katika klabu hiyo Juni mwaka jana amemuonyesha kisogo Ozil kwa madai kuwa hana imani kama atamudu mfumo wake na kwa sababu hiyo haoni haja nyota huyo kuendelea kuwapo katika klabu hiyo.
Inter Milan ambao walikaribia kuinasa saini yake nao wamebadili upepo wameweka wazi kuwa hawamtaki na hawana mpango naye.
Emery anaamini Arsenal inaweza kushinda mataji bila Ozil hivyo wapo tayari afungashe virago aondoke.Ni uamuzi wake aondoke sasa au baadae lakini kocha amtaki.
Taarifa zinaonyesha kuwa kwa sasa Ozil ameanza kuungwa mkono na mashabiki katika bifu lake na Emery na kama hali itakuwa kama ilivyo huenda akashinda kwa nguvu za nje ya uwanja.
Mashabiki hawaonyeshi kufurahishwa na kitendo cha Ozil kuwekwa benchi kwani hata katika mchezo wa Ligi ya Europa dhidi ya BATE uliochezwa Alhamisi iliyopita ambao Arsenal ilifungwa bao 1-0, baadhi yao walikuwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe uliotaka Emery atimuliwe.
Lakini Mhispania huyo anadai hawezi kumtumia Ozil katika michezo muhimu inayohitaji ushindi kwa maneno mepesi hana msaada.
Licha ya kikosi cha Emery kuwa imara zaidi eneo la ushambuliaji akiwamo Ozil wakati timu hiyo ilipopata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Leicester City, lakini Emery anasema vijana wake wanaweza kufanya makubwa bila uwepo wa nyota huyo mwenye jezi namba 10.
Katika mchezo dhidi ya West Ham, Ozil anadaiwa alifanya mandalizi kabambe wiki mbili kabla ya mchezo lakini mwisho wa siku akajikuta hayupo hata kwenye benchi la wachezaji wa akiba.
Lakini huu unafahamika kama mpango maalumu kwa Emery kulazimisha kiungo huyo aondoke.
Mara ya mwisho kucheza kikosi cha kwanza ilikuwa wiki sita zilizopita katika mchezo dhidi ya Brighton tangu hapo Ozil ametumika mara mbili kikosi cha Arsenal.
Katika mchezo dhidi ya Brighton nyota huyo aliondolewa kipindi cha kwanza na ilimlazimu kukaa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja akisubiri apangwe tena katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Manchester United ambao Arsenal ilifungwa mabao 3-1.
Nyota huyo alipoanza katika kikosi cha Arsenal dhidi ya Cardiff City wiki mbili zilizopita Arsenal ilishinda mabao 2-1.
Emery alimweka tena benchi katika mchezo dhidi ya Manchester City licha ya Mhispania huyo hudaiwa kujali zaidi uwezo wa mchezaji katika kila mchezo lakini hakutaka kuangalia alichokifanya Ozil dhidi ya Cardiff City.
“Nadhani ni suala gumu lakini sidhani kama linausu kiwango cha mchezaji.Nafikiri Arsenal wanataka kupunguza matumizi ya fedha na hiyo inaonekna kuwa na maana kwao,”anasema kiungo wa zamani wa Liverpool, Joe Cole.
“Kwa miaka mingi Arsenal, ikiwa chini ya Arsene Wenger imekuwa na tabia kama hii.Kocha anatakiwa kutumia wachezaji bora alionao wakati anapowahitaji na Ozil ni mmoja kati ya nyota ndani ya kikosi.
“Kama utawauliza Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyanga kuhusu kucheza pamoja na Ozil watasema ndio wapo tayari, hivyo ni jambo la ajabu kumuona akiwa nje ya uwanja,”alisema.
Mkongwe wa Manchester United, Andy Cole anafananisha kitendo kinachomtokea Ozil sasa hivi ni kama mchezo wa kuigiza.
Ozil alikuwa katika afya nzuri ya mchezo kabla ya Arsenal kusafiri kucheza michuano ya Ligi ya Ueropa ambao washika mtutu hao walifungwa bao 1-0 dhidi ya BATE Borisov Alhamisi iliyopita.
“Huu ni mchezo wa kuigiza.Tunafahamu uwezo wake,”anasema Cole.
Klabu ya Arsenal sasa ina haha kumtafutia Ozil timu ya kwenda kucheza kwa mkopo lakini mtihana wanaoupata ni ukubwa wa mshahara.
Arsenal kwa sasa haipo tayari kuendelea kumlipa Ozil pauni milioni 18 kila msimu.
Ingawa Arsenal inafanya jitihada za kumtafutia Ozil klabu kwa mkopo lakini kiungo huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani hataki kuondoka kwa mkataba wa muda mfupi.
Paris Saint Germain ilitaka kumsajili Ozil kwa mkopo wa muda mfupi katika usajili mdogo wa Januari mwaka huu lakini alikataa.
Kinachotokea kwa Ozil akiwa Arsenal ndicho Emery alikuwa akikifanya dhidi ya Neymar Jr pale PSG.
Emery na Neymar walikuwa katika mgogoro uliotokana na nguvu aliyokuwa nayo Mbrazil wakati akitua PSG kwa dau la kuvunja rekodi.
Kinachotokea katika vyumba vya kubadili nguo timu ya Arsenal ni sehemu ya kilichokuwa kikitokea PSG lengo likiwa kumfanya Neymar kukosa utulivu.
Emery hataki kumpa Ozil nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya klabu ya Arsenal kama ilivyokuwa kwa Neymar katika klabu ya PSG.
Tayari Emery amesema Ozil si mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Arsenal na wachezaji wengine wanahisi hataweza kubadili uwamuzi wake kwa kuogopa kuathiri hali ya hewa ndani ya vyumba vya kubadili nguo ingawa nyota katika kikosi hicho wanaamini wanamuhitaji Mjerumani huyo kwa sasa.