LONDON, ENGLANDÂ
LIGI Kuu nchini England, imethibitisha kuwa wachezaji na viongozi nane wanaoshiriki Ligi hiyo wamekutwa na maambukizi ya virusi vya corona baada ya kufanyiwa vipimo wiki iliopita.
Jumla ya wachezaji pamoja na viongozi 1,575 walifanyiwa vipimo kuanzia Jumatatu ya Oktoba 12 na Oktoba 18, kati ya hao nane wamekutwa na maambukizi.
Idadi hiyo inaonekana kuzidi ya wiki moja iliyopita ambapo watu wenye maambukizi walikuwa watano, lakini safari hii namba ya idadi imezidi kuwa kubwa.
Kutokana na hali hiyo, wachezaji na viongozi hao waliokutwa na maambukizi wametakiwa kukaa karantini kwa siku 10, hivyo hawatakiwi kujihusisha na maandalizi yoyote ya timu zao kwa kipindi cha siku 10.
Ilikuwa wiki ya wachezaji mbalimbali kuwa kwenye mapumziko ya Ligi Kuu na kujiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya kalenda ya FIFA, hivyo wachezaji wengi wamekutwa na maambukizi mara baada ya kurudi kuyatumikia mataifa yao.
Jumapili ya wiki iliopita uongozi wa klabu ya Crystal Palace ilimtangaza mshambuliaji wake Jordan Ayew kuwa amekutwa na maambukizi ya virusi vya corona mara baada ya kurudi kuitumikia timu yake ya taifa ya Ghana.
Beki wa pembeni wa timu ya Burnley, Phil Bardsley, hakuwepo kwenye mchezo dhidi ya West Brom ambao ulimalizika bila ya kufungana na inadaiwa kuwa, mchezaji huyo ni kati ya wachezaji nane wenye maambukizi ya virusi vya corona.
Ligi Kuu England inatarajiwa kuendelea Ijumaa wiki hii ambapo Aston Villa watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani huku wakiwakaribisha Leeds United ambao wamepanda daraja msimu huu. Michezo mingine itaendelea Jumamosi kwa michezo minne West Ham wakiwa nyumbani kupambana na Man City, huku Crystal Palace wakiwafuata Fulham, wakati huo Man United wakiwa Old Trafford kupambana na Chelsea, Liverpool watawakaribisha Sheffield United.