Na BRIGHITER MASAKI
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wamefungulia, udahili wa wanafunzi katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa kozi zote zinazotolewa na vyuo vya elimu ya Ufundi, wameanza rasmi Juni 15, 2020 hadi Septemba 15 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, mapema leo, jijini Dar es salaam, Mkurugenzi, Uthibiti, Ufuatiliaji na Tathimini, Dk Jofrey Oleke, amesema dirisha hilo limefunguliwa leo, Vyuo vinaruhusiwa kupokea maombi ya udahili kwa waombaji wenye sifa.
“Vyuo vinaruhusiwa kupokea maombi ya udahili kuanzia leo (jana) Juni 15 hadi September 15, 2020, Vyuo hivyo vitachagua waombaji wenye sifa kati ya tarehe 16 hadi 21 Septemba, 2020 na kisha tarehe 22 hadi 29 Septemba 2020,”
“Majina ya waombaji waliochaguliwa yatawasilishwa NACTE kwa ajiri ya uhakiki, majina yaliochaguliwa na kuhakikiwa na NACTE yatatangazwa na vyuo husika Octoba 8, 2020, kwa ajili ya kuanza masomo Novemba 16 mwaka huu” amesema Dk Oleke.
Aidha waombaji wa programu za afya kwenye Vyuo vya Serikali watatuma maombi yao moja kwa moja kupitia tovuti ya Baraza (NACTE) kuanzia leo (Juni) 15 Juni, 2020 hadi tarehe 15 Agosti, 2020, Majina yatakayochaguliwa yatatangazwa tarehe 26 Agosti, 2020.
Aliongeza kuwa baraza linawashauri waombaji na wazazi kuhakikisha kuwa wanaomba kwenye Vyuo ambavyo vimeorodheshwa.