27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mwijage, Tizeba wang’olewa uwaziri

Na Aziza Masoud -Dar es Salaam


RAIS Dk. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kutengua uteuzi wa mawaziri wawili; wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba na wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Mbali na kutengua uteuzi wa mawaziri hao, Rais Magufuli amewapandisha naibu mawaziri wawili kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wizara naibu waziri mmoja huku akiwateua naibu mawaziri watatu wapya akiwamo Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.

Waliopandishwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ambaye sasa anakuwa Waziri wa Kilimo akichukua nafasi ya Tizeba.

Mwingine ni aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Kakunda ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji akichukua nafasi ya Mwijage.

Kwa taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa, naibu mawaziri wapya mbali na Waitara aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Kakunda, mwingine ni Constantine Kanyasu ambaye amekuwa Naibu  Waziri wa Maliasili na Utalii akichukua nafasi ya Hasunga.

Pia Innocent Bashungwa ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo akichukua nafasi ya Mary Mwanjelwa ambaye amepelekwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, uteuzi wa mawaziri na manaibu hao umeanza jana na wataapishwa kesho saa tatu asubuhi.

Aidha Rais Magufuli pia ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Anna Abdallah na kuivunja bodi hiyo kuanzia jana.

Taarifa hiyo ya Ikulu haikueleza sababu za rais kuchukua uamuzi huo ambao umekuja katika wakati ambao kuna mvutano wa bei ya korosho baina ya wafanyabiashara na wakulima wa zao hilo.

Oktoba 28 mwaka huu, gazeti hili liliandika habari ya uchambuzi ikieleza jinsi Dk. Tizeba alivyo katika hatari ya kupoteza uwaziri wa kilimo kutokana na mvutano uliokuwa unaendelea juu ya bei stahiki itakayotumika kununua zao hilo kwa wakulima.

Dalili za Tizeba kupoteza uwaziri zilianza kuonekana baada ya Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Profesa Wakuru Magigi kung’olewa wadhifa huo huku msingi ukiwa ni suala la bei kuleta mvutano mkubwa.

Uchambuzi wa gazeti hili ulibaini viashiria kuwa huenda kutumbuliwa kwa Profesa Magigi ilikuwa ni kuandaa mapito ya kutenguliwa kwa Dk. Tizeba ambaye wizara aliyoiongoza ilionekana kunyoshewa vidole na wadau wengi wa sekta ya kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles