25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU AMALIZA MGOGORO MORAVIAN

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


HATIMAYE Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amemaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka mitano ndani ya Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Mashariki.

Mgogoro huo ambao unatajwa kusababisha madhara makubwa na kuumiza wengi kiroho ndani ya kanisa hilo, ulianza tangu mwaka 2013 baada ya mkutano wa kanisa (Sinodi) kuchagua Halmashauri Kuu ya Jimbo ambayo inaongozwa na Mchungaji Samwel Mwaiseje.

Msingi wa mgogoro huo ulianza baada ya wale ambao hawakufika kwenye Sinodi hiyo kuhoji ni kwanini waliachwa nje.

Akizungumza jana mbele ya mkusanyiko wa waumini wa kanisa hilo, Mwigulu alisema muumini au kiongozi wa Moravian ambaye hataki kufuata taratibu za kanisa hilo aondoke.

Alisema wakiona kiongozi hatoshi wamwondoe kwa utaratibu na endapo wakifanya fujo atamtumia Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).

“Muwe na utaratibu wa kimoravian, ambaye hataki kufuata utaratibu aondoke. Mnatakiwa mjitafakari kwanini mmefikia hapo kwenye mgogoro.

“Huwezi kuwa muumini wa Moravian na kukataa kufuata taratibu za Moravian. Kwetu sisi image ya taasisi ni jambo la muhimu kuliko mtu mmoja mmoja,” alisema waziri huyo.

Alisema ni aibu kubwa kuwapo kwa migogoro katika nyumba za ibada na kwamba si sifa kwa mtu kuitwa huyu ni wa upande fulani.

Alisema ni lazima watunze heshima kwa yule wanayemwabudu kwa sababu Yesu Kristo habadiliki na kanisa litaendelea kuwepo lakini viongozi wote watapita.

 “Hivi kweli mko rohoni ninyi kugombania uongozi makanisani na kuacha ibada zisifanyike? Kwanini mnachukiana kwa sababu ya mambo yasiyo ya kudumu? Hii migogoro ya uongozi makanisani, ni vitu vidogo sana tena vya kupita.

“Hivi hawa waliokuwa wakigombana, ikitokea watoto wenu wakakutana chuo kikuu wakapendana, mahari mtapokelea wapi? Mnawekeana hata mipaka ya kupita, je, siku mkikutana kwa Mungu mtawekeana mipaka,” alihoji Mwigulu.

Mwigulu ambaye pia ni Mbunge Iramba Magharibi, aliwataka waumini hao kutafuta njia ya kuyamaliza yale wanayotofautiana na kwamba wayamalize kiroho.

“Huwa makanisa na misikiti humuombea rais lakini mnawezaje kumuombea rais, wakati mna vitu rohoni,” alisema.

Aidha, Mwigulu alisema alipofika Wizara ya Mambo ya Ndani, alikuta magari ya washawasha mengi yamenunuliwa kwa ajili ya kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, lakini hayakutumika kwa sababu kulikuwa kuna amani.

“Nilipofika Mambo ya Ndani nilikuta magari ya washawasha yaliyowekwa kutumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka juzi lakini hayajatumika. Hii ni kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa dini kuliombea Taifa,” alisema Mwigulu.

Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania, Kenan Panja, alisema mpasuko huo ulikuwa kama ajali na kwamba wengi wasingependa kuona tatizo hilo likiendelea ndani ya kanisa hilo.

“Ofisi yangu kipindi chote cha mgogoro imekuwa ikiwasiliana na upande wa pili kuona namna gani wanaweza kulirejesha kanisa pamoja kwa nia moja, kanisa la undugu Tanzania na duniani kote,” alisema askofu huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles