STAA wa filamu ya ‘Hotel Rwanda’ inayozungumzia mauaji ya Kimbari ya Rwanda, Paul Rusesabagina, amefunguliwa mashitaka ya ugaidi nchini humo.
Katika filamu hiyo, Rusesabagina mwenye umri wa miaka 67 ameigiza kuwa ni shujaa aliyekuwa akiokoa maisha ya watu wakati wa vita hiyo ya mwaka 1994.
Ndani ya siku 100 za vita hiyo kati ya makabili mawili, Wahutu na Watutsi, watu 800,000 walipoteza maisha lakini Rusesabagina alipongezwa kwa namna alivyookoa vifo vingi.
Hata hivyo, alianza kuingia kwenye uhasama na Serikali pale tu alipoanza kukosoa kile alichoona hakikuwa sahihi kutoka kwa utawala wa Rais Paul Kagame.
Kwa mujibu wa mashitaka yanayomkabili, Rusesabagina anashutumiwa kwa kukisaidia kikundi cha waasi kilichoua raia tisa wasio na hatia mwaka 2018.