*Asema Watanzania wako nyuma ya jitihada zake…
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT)Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha uzinduzi wa filamu ya ‘Royal Tour’ na kusisitiza kuwa Watanzania wote wapo nyuma ya jitihada zake anazozifanya kulitangaza Taifa la Tanzania Duniani.
Akizungumza ikiwa ni siku moja tangu kuzinduliwa kwa filamu hiyo uliofanyika jijini Arusha jana, Kevela amesema kwa kufanikisha hatua hiyo, Rais Samia anazidi kuonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kuiletea maendeleo Tanzania.
”Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ukweli anazidi kufanya mambo makubwa kwa Taifa hili kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani, Mungu aendelee kumlinda na kumsimamia,” amesema Kevela.
Amesema kuzinduliwa kwa filamu hiyo inayoonyesha vivutio mbalimbali vya utalii na kitamaduni, kutazidi kuongeza idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini kwa lengo la kuja kuvitazama hatua ambayo itasaidia kukuza pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni.
Aidha, Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart amewataka Watanzania wote kwa umoja wao kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ili aweze kutimiza malengo yake ya kuiletea nchi maendeleo jambo ambalo pia litawezesha kuongezeka kwa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Awali, kabla ya kuzinduliwa kwa filamu hiyo nchini, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa nchini Marekani aliposhiriki uzinduzi wa filamu hiyo ya Royal Tour aliyoshiriki kuicheza katika Majiji mawili ya New York na Los Angels, uzinduzi ambao ulioudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo mashuhuri.
Saa chache kabla ya uzinduzi huo wa Marekani, Rais Samia pia alishiriki mkutano na baadhi ya watu maarufu uliofanyika kwenye klabu ya faragha ya Lotos uliopo New York ambapo miongoni mwa waliohudhuria ni Meya mashuhuri wa jiji la New York, Eric Adams, ambaye ameeleza kuipenda Tanzania na kuahidi kuitangaza zaidi katika jiji lake la New York.
Mtu mwingine mashuhuri aliyehudhuria ukiondoa mabilionea na wamiliki wa makampuni makubwa duniani ikiwemo watangazaji wa CNN, CBS nk alikuwa ni Gayle King mtangazaji mashuhuri wa vipindi vya CBC Mornings na “King in the House”
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisema matarajio mara baada ya kuzinduliwa, idadi ya watalii nchini itaongezeka mara mbili zaidi ya ilivyo sasa na kuliongezea Taifa mapato yatokanayo na sekta ya utalii.
Alisema kwa namna kazi inavyofanyika, Tanzania itegemee kuongeza idadi ya watalii watakaoingia nchini na kuwataka watu waliopo katika sekta hiyo kujipanga vyema kuwapokea wageni hao na kuwahudumia kwa ajili ya kuwafanya waweze kuongeza siku za kukaa nchini.