28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mwenyekiti UWT atamani viti maalumu bungeni viongezwe

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Gaudentia Kabaka, amesema anatamani nafasi za wabunge wa viti maalumu ziongezeke bungeni kuliko ilivyo sasa.

Amesema hali hiyo itasaidia kustawisha usawa wa kijinsia kwa kuwa na uwakilishi sawa kati ya wanaume na wanawake ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Kabaka ametoa kauli hiyo, wakati kukiwa na msukumo katika jamii kupinga uwepo wa viti hivyo bungeni, kwa madai kuwa wabunge hao ni ‘mzigo’ kwa taifa, kwani wabunge wa majimbo wanatosha.

Akizungumza na MTANZANIA hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu, Kabaka alisema licha ya changamoto kadhaa wanazokutana nazo wanawake katika kuwania nafasi za kisiasa, lakini bado haiondoi haki ya wanawake kuchaguliwa na kuingia kwenye vyombo vya maamuzi.

“Katika hili ukiniuliza mimi kama Mwenyekiti wa UWT kama inawezekana ninaomba tu nafasi hizi ziongozeke ili kupata uwino sawa na wanaume ndani ya vyombo vya kutunga sheria ikiwamo mabaraza ya madiwani na Bunge.

“Wanawake ndiyo watu wanaoguswa na matatizo yaliyopo katika jamii moja kwa moja, ukizungumzia maji, afya, elimu hapo mwathirika mkubwa ni mwanamke, hivyo sauti yao bungeni ni muhimu.

“Ni wanawake wangapi wenye uwezo wa kushindana na wanaume majimboni na wakashinda kwa kiwango kikubwa? Hata ukiangalia baadhi ya makabila bado wanamtazamo hasi dhidi ya mwanamke, bila viti maalumu bungeni sauti ya wanawake itapotea,” alisema Kabaka.

Licha ya hali hiyo alisema kuwa suala ubunge wa viti maalumu ni suala la kikatiba ingawa linategemea idadi ya kura alizopata mgombea urais na kura za wabunge wa majimbo.

Alipoulizwa kama anaridhishwa na utendaji wa wabunge wa viti maalumu hasa watokanao na CCM, alisema anaridhika nao kwani wengi wao wamekuwa wakijenga hoja kutokana na maeneo wanayotoka na hasa zinazohusu jamii.

Akizungumzia suala la ukomo wa ubunge wa viti maalumu kama ilivyopendekezwa kwenye kanuni za CCM miaka ya nyuma, alisema suala hilo limeondolewa na halipo tena na wabunge wanaopenda kwenda kuwania ubunge wanaruhusiwa wakati ukifika.

KUCHA BANDIA BUNGENI

Mwenyekiti huyo wa UWT, aliungana na uamuzi wa Spika wa Bunge alioutoa hivi karibuni wa kuzuia wanawake wanaoweka kucha, nywele na kope bandia.

Alisema Spika ni kiongozi wa mhimili kamili wa Bunge na hadi kufikia kutoa uamuzi huo ameona kuna mambo yanakwenda kinyume cha utaratibu na maadili ya Mtanzania.

Kabaka alisema wabunge wanawake wanatakiwa kujitathmini wenyewe kuhusu mienendo yao ndani ya Bunge kwa mavazi na mapambo.

Alisema Bunge ni chombo kinachoheshimika kutokana na kazi zake nyeti na nzito kwa nchi hasa katika utungaji wa sheria pamoja na kuwa sehemu ya kusemea matatizo ya Watanzania wote.

“Tunahitaji kuwa na wabunge ambao wako sawasawa na si kuvaa vibaya. Hata sisi wakati tupo tunasomea ualimu chuoni na tulipokuwa tunafundisha tulikatazwa kuvaa viatu virefu pamoja na kupaka lipshine. Lakini siku hizi yamekuwa yakifanyika kwa hiyo hakuna maadili kabisa.

“Ingawa mambo mengine hayapo kwenye kanuni za Bunge lakini sasa umefika wakati yaangaliwe yaingizwe kwenye kanuni.

“Huwezi kuwa na wabunge wanavaa ovyo, mbona kwenye mavazi kanuni zimewekwa wazi ni mavazi gani kwa mbunge anayotakiwa kuvaa sasa na haya mengine inawezekana vipi wabunge hasa wanawake washindwe kuyaona wenyewe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles