Na MWANDISHI WETU-TABORA
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James, amesema kuwa wananchi wanaopata bahati ya wabunge wao kupewa majukumu mengine ya kiserikali ni vema wakaendelea kupewa ushirikiano.
Hayo aliyasema jana mkoani Tabora, alipozungumza akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa ndani katika Kijiji cha Nkiniziwa kilichopo Halmashauri ya Nzega Vijijini mkoani hapa.
Alisema lengo la chama kuisimamia Serikali ni kutaka kuendeleza msingi wa chama kuaminiwa na wananchi ili CCM iendelee kubaki madarakani kwa ridhaa yao kutokana na kuwajali na kuwatumikia waliowapa ridhaa.
“Tunatakiwa kufanya kazi kwa nguvu moja ili kuendelea kuaminiwa na wananchi. Haiwezekani Rais (John Magufuli) akose usingizi kwa kuwafikiria wananchi, huku ishindikane madiwani, wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa washindwe kutatua kero za wananchi vijijini.
“Jambo hili halikubaliki hata kidogo, ni lazima watimize wajibu wao pia katika maeneo yao kwa kuhakikisha maendeleo yanafanyika kwa kushirikiana na wananchi,” alisema James.
Alisema iwapo viongozi wa chama na Serikali hawatashughulikia shida na matatizo ya vijana na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati, kuna hatari siku moja wakaja kukataliwa pindi wanapokuwa wanahitaji ridhaa ya wananchi.
“Heshima yetu inatokana na kuaminiwa kwa CCM kuendelea kushika dola. Hutaweza kubaki na heshima hii ikiwa tutakosa madaraka yanayotokana na ridhaa ya wananchi ambao tumaini lao siku zote ni CCM,” alisema.
Alisema ikitokea kiongozi mmoja kuteleza au kukosea kwa bahati mbaya, ni wajibu kwa viongozi wengine kumwita na kukaa naye na kumshauri sambamba na kumsahihisha kwa mujibu wa utaratibu wa CCM badala ya kuwekeana chuki na vinyongo.
“Nguvu ya chama chetu ni watu. Watu wenyewe ni hawa masikini, wanyonge, wakulima na wafanyakazi. Tusipohangaika na matatizo yao na kuwatatulia watatupuuza, wakitupuuza tutapoteza heshima yetu na chama hakiko tayari jambo kama hilo litokee,” alistitiza James.
Katika msafara huo James ameambatana na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia Mwita, Kaimu Katibu Mkuu, Shaka Hamdu Shaka, Kaimu Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi, Jokate Mwegelo na Kaimu Katibu Idara ya Oganaizesheni, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Mohamed Abdallah.