Na PETER FABIAN
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amewaagiza maofisa ardhi wa Manispaa ya Wilaya ya Ilemela kuacha kuwabagua baadhi ya wananchi katika upimaji shirikishi na urasimishaji makazi kwa kisingizio cha kutokamilisha kulipia gharama za upimaji ardhi.
Mabula ambaye ni Mbunge wa Ilemela (CCM), alitoa agizo hilo alipohudhuria kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Ilemela.
Aliwataka maofisa hao kuwapimia wananchi wote bila ubaguzi hata kama hawajakamilisha malipo kuondoa usumbufu utakapozinduliwa mpango kabambe wa Jiji la Mwanza.
“Wizara imeelekeza kupima kila kipande cha ardhi nchini, hivyo naomba maofisa ardhi wa Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza kutekeleza hatua hii haraka.
“Hakikisheni mmepima maeneo yote ya ardhi ya
wananchi kabla ya kuzinduliwa hivi karibuni mpango kabambe ambao umelenga pia Mwanza kuwa jiji la kisasa,”alisema.
Mabula alisema baada ya kuzinduliwa mpango huo hakutakuwa na upimaji ardhi shirikishi tena kwa utaratibu wa sasa.
Alisema kwa sababu hiyo ili wananchi wasilalamike ni vema wakapimiwa ardhi kwenye mitaa yao kabla ya
wizara kuuzindua rasmi mpango huo hivi karibuni.
“Wananchi wamenilalamikia kama mbunge kuwa wamekuwa wakirukwa na kubaguliwa kupimiwa na maofisa ardhi kwa kisingizio kuwa hawajakamilisha uchangiaji fedha urasimishaji makazi katika mitaa ya Ibungilo na Kiloleli.
“Hebu wapeni elimu kuwa waendelee kulipa hata kidogo kidogo hadi watakapomaliza siyokukataa kuwapimia,”alisisitiza.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Wanga aliahidi kulisimamia suala hilo lililojitokeza .
Alisema agizo hilo atalisimamia kwa kukaa na
wataalamu wake wa Idara ya Mipango Miji na Ardhi na kitengo cha upimaji kuhakikisha hakuna mwananchi atakayetoa malalamiko ya kutopimiwa eneo lake hata kama hayupo.
Naye Meya wa Manispaa hiyo, Renatus Mulunga (CCM) alisema ataangalia uwezekano wa kuwasamehe wazee wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za upimaji shirikisi katika urasimishaji makazi.