Na JANETH MUSHI-ARUSHA
HATIMAYE mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi, ameachiwa kwa dhamana jana baada ya kuhojiwa.
Lihundi aliachiwa jana saa 9:20 alasiri baada ya kuwekwa rumande kwa zaidi ya saa 24 tangu juzi Desemba 21, mwaka huu saa 8 mchana katika kituo cha Polisi cha Usa river, wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.
Aliwekwa rumande kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, aliyedai kuwa amekuwa akiandika habari za uchochezi.
Baada ya mwandishi huyo kuachiwa, shangwe zilitawala kutoka kwa wanahabari wenzake wa Mkoa wa Arusha ambao walifika kituoni hapo kujua hatima yake.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa kwa dhamana, Liundi alisema katika mahojiano kati yake na polisi alidaiwa kuripoti habari za migogoro ya ardhi na maji ambazo hazikumfurahisha DC Mnyeti.
“Habari nyingine ninazodaiwa kuripoti ni za kipindi cha wakuu wa wilaya waliopita, ambazo nyingi ni za migogoro ya wananchi, hivyo inaonekana taarifa za wananchi hazitakiwi wakati taarifa nyingi hata Rais John Magufuli, anaziona kwenye vyombo vya habari na kutolea uamuzi ikiwamo suala la wamachinga.
“Sijajengewa hofu, nasikia natafutwa hata Wilaya ya Ngorongoro na nitakwenda, nitawekwa ndani hata mara 200, lakini sitaogopa wala kurudi nyuma, kwani taarifa hizo nyingi huwa kuna viongozi kama madiwani na wenyeviti wa vijiji, ila naona hawaruhusiwi kuongea zaidi ya uongozi wa wilaya,” alisema
Aliwataja wakuu hao wa wilaya waliopita ambao anadaiwa katika kipindi chao alikuwa akiripoti habari hizo za uchochezi kuwa ni Hasna Mwilima ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia CCM na Wilson Nkumbaku aliyetenguliwa uteuzi wake na Rais Magufuli.
“Nawashukuru waandishi wenzangu kwa ushirikiano huu kwani suala hili halikwepeki, mwandishi yeyote anaweza kuwekwa ndani na nitaripoti taarifa yoyote kwani kila ngazi ya uongozi inahusika na wangekuwa hawatakiwi wasingekuwapo kisheria,” alisema.