Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Aliyewahi kuwa Mwandishi wa Habari wa Magazeti ya Mtanzania na Rai ya kampuni ya New Habari(2006) na baadae kujiunga na magazeti ya Tanzanite, Evance Magege amefariki dunia jioni ya Mei 23, 2022 jijini Dar es Salaam.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa Magege alifariki ghafla nyumbani kwake Mbezi Mpigi Magohe jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia msiba huo aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Rai, Jimmy Charles amesema Magege atakumbukwa kwa mengi ikiwamo ucheshi wake na uchapakazi.
“Magege alikuwa ni mtu mchapakazi ambaye nimefanya nae kazi nikiwa Mtanzania na hata nikiwa Rai alikuwa miongoni mwa watu wanaopenda kunishauri na kuandika pale anapoona anapenda kuandika huyo ndiye Magege ninayemjua.
“Na hata wakati anaoa nadhani nilishiriki kwenye harusi yake, kimsingi kifo chake kimenisikitisha sababu ameondoka akiwa bado kijana na mwenye ndoto nyingi, pia familia yake sasa imemkosa baba, baba amepotea mapema mno, hivyo tutazidi kumuombea,” amesema Charles ambaye kwa sasa ni Mhariri Mtendaji wa Jarida la Panaroma.
Upande wake aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Mtanzania, Kulwa Karedia, amesema taifa limepoteza kijana mdogo ambaye bado taifa lilikuwa likimhitaji.
“Kwa kweli nimesikitika sana sababu Magege alikuwa ni kijana mchapa kazi na hakuwa na makuu na mtu, taifa lilikuwa linamhitaji na familia yake ilikuwa inamhitaji, ni pigo kwa tasnia ya habari kwa ujumla,” amesema Kulwa Karedia.
Msiba wa Magege upo Mbezi Mpigi Magohe na taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi zitatolewa baadae.