Scholastica Wilson,Dar es Salaam
Mwanamuziki wa muziki wa dansi, Ally Choki ametolewa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) alikowekwa jana baada ya hali yake kuwa mbaya, kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Jijini Mwanza wakati akisubiriwa kaka yake.
Ally Choki alikimbizwa ICU baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Kisukari na Presha.
Kaka wa mwanamuziki huyo, amesema hali ya mdogo wake ilikuwa mbaya na ilihitaji usaidizi wa karibu mno ndiyo maana amelazimika kwenda huko anatarajiwa kufika leo.
Kaka huyo amesema kama hali ya ndugu yake itaonyesha kutotengamaa atalazimika kumuhamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Hamad Choki amesema Ali Choki alianza kujisikia vibaya Ijumaa iliyopita na kabla ya kukimbizwa katika hospitali hiyo alifikishwa hospitali binafsi jijini humo.
Amesema alipofikishwa Bugando ndugu yake huyo alikosa hewa hivyo akawekewa hewa ya Oxgen na kisha akawekwa chumba cha wagonjwa mahutiti (ICU).
“Hali ya Choki siyo nzuri kutokana na sukari kupanda ghafla lakini presha yake imejichomoza zaidi ingawa bado madaktari wanaendelea kumsaaidia kuona namna ya kumrejesha katika hali yake ya kawaida,” amesema Hamad.
Kaka huyo wa Ali Choki anawaomba wadau wa muziki wa dansi na Watanzania kwa ujumla wamuombee mwanamuziki huyo ili apone haraka na aweze kurejea kwenye bendi yake mpya ya Super Kamanyola ya jijini Mwanza.