23.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAMKE NYUMA YA MAFANIKIO YA MWANAUME

Na ATHUMANI MOHAMED

SUALA la kuingia kwenye muunganiko wa ndoa katika maisha ni jambo lenye heshima, hadhi na furaha. Lakini zaidi ya yote, ni sehemu muhimu ya mchakato wa kawaida katika maisha ya binadamu.

Hapa namaanisha kuwa, kuingia kwenye ndoa ni sehemu ya maisha ya binadamu hivyo basi inahusika moja kwa moja hata katika mambo ya mafanikio kimaisha.

Ukweli ni huu. Walio kwenye ndoa, hasa zenye masikilizano wana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa maishani mwao kuliko wale ambao hawana ndoa. Kuna uhusiano wa karibu sana katika kujenga familia na mafanikio ya kimaisha na ndoa.

Kwa bahati mbaya sana, siku hizi vijana wengi ni kama hawaoni umuhimu sana wa suala la kuoa au kuolewa. Leo katika mada hii nitazungumza kwanza na wanaume tu. Wanawake nawaweka kiporo hadi siku zijazo.

Zipo sababu kadhaa ambazo zinawafanya vijana kuchelewa au kupuuzia kuoa, mwisho wanakuja kushtuka tayari umri unakuwa umekwenda. Yapo madhara makubwa yanayotokana na kuchelewa kujenga familia.

Katika mada hii nitagusia mambo ya msingi zaidi juu ya kutokuingia kwenye ndoa mapema (kwa wanaume tu).

SUALA LA UMRI

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaeleza kuwa kijana wa kiume, akifikisha umri wa miaka 18 ana uhuru wa kuoa na kuanza kuishi maisha ya kinyumba. Lakini kwenye dini, haifafanui moja kwa moja kuhusu umri, ingawa kuna mistari inafafanua kwenye Biblia na Quran juu ya muda wa uchumba na ndoa kwa maisha ya binadamu kama jambo la lazima.

Kwa maisha ya kileo, ni sahihi zaidi kijana wa kiume angalau mwenye umri wa kuanzia miaka 22 – 30 awe ameshaingia kwenye ndoa na kuanza kutengeneza maisha yake.  Kwa kuwa leo tunazungumzia kuhusu kijana wa kiume kwanza, maelezo haya yanaweza kutosha.

ZIPO FAIDA ZA KUOA MAPEMA

Faida kubwa zaidi katika kuoa mapema, ukiacha mengine yote ni kupata muda wa kutosha wa kulea watoto wakati ukiwa na nguvu. Watoto wa kuwazaa ukiwa na umri mkubwa, mara nyingi huwa wanadhulumiwa malezi na mahitaji sahihi.

Mfano, ikiwa baba atazaa mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 40, maana yake hi hii: Mtoto akiwa na umri wa miaka sita, ambao ndiyo huanza darasa la kwanza, baba atakuwa na umri wa miaka 46. Atamaliza darasa la saba akiwa na miaka 13 huku baba akiwa na 51.

Ongeza miaka sita ya kidato cha kwanza hadi cha sita, mtoto atakuwa na miaka 20 (ukiweka kipindi cha kusubiri matokeo) baba atakuwa na miaka 58 – huo ni muda wa kijana kujiunga na Chuo Kikuu. Hapo sijazungumzia watoto wengine wanaofuata.

Maana yake, mzee huyu mwenye miaka 58 bado atakuwa na mzigo wa kusomesha. Katika umri huo ambao wengi wanakuwa wameshastaafu kazi, uwezo wa ubunifu wa biashara au usimamizi wa biashara unakuwa mdogo, haiwezi kuwa rahisi kwake kuwaendeleza sawasawa watoto wake kielimu.

Lakini ukioa mapema, unakuwa na uwezekano pia wa kupata watoto mapema, ambao utakuwa na uwezo wa kuwasomesha ukiwa na nguvu na kuwafuatilia vizuri kwenye elimu yao ambayo kimsingi ndiyo msingi wa maisha.

Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam. Nakualika tena wiki ijayo katika sehemu ya pili, USIKOSE!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles