JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA,
MATUMIZI ya watoto wanamitindo daima yamekuwa suala lenye utata, wengi wakilihesabu kuwa mwiko kutokana na hofu ya kuathiri makuzi yao, wengine wakiona ni sawa tu.
Miaka 12 nyuma, unakumbukwa katika ulimwengu wa mitindo baada ya kuibuka mwanachama mpya mdogo kabisa katika fani hiyo, Thylane Blondeau.
Muibuko wa dogo huyo katika ulimwengu huo, akiwa na umri wa miaka minne tu, ulishuhudia akitajwa kuwa msichana mrembo kuliko wote duniani.
Wazazi wake ni staa, wakiwa miongoni mwa wenzi maarufu nchini humo; baba akiwa mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa timu ya Taifa na klabu ya AS Monaco, Patrick Blondeau na mama muigizaji Véronika Loubry.
Kwa sababu hiyo mtoto wa nyoka ni nyoka!, ni kana kwamba amerithi ustaa kutoka kwa wazazi wake.
Mjulikano wake huo duniani kipindi hicho ulitokea wakati aliposhiriki onesho la mitindo la mbunifu maarufu wa mavazi Ufaransa, Jean Paul Gaultier.
Katoto Thylane Lena-Rose Blondeau kakawa moja kwa moja kastaa katika umri wake huo mchanga na miaka sita baadaye katika hali iliyozua utata akazipamba kurasa za jarida maarufu la Ufaransa, Vogue. Hiyo ilikuwa mwaka 2011 wakati akiwa na umri wa miaka 10.
Alikuwa mwanamitindo mdogo kabisa kuwahi kuonekana katika jarida hilo na baadhi hawakukubaliana na uzito wa vipodozi na nguo alizotokea nazo.
Watu wengi walililaani jarida la Vogue kwa kumweka Thylane katika namna ya kutamanisha kimapenzi, akiwa amejipodoa vilivyo na kuvalia mavazi na cheni nzito ya dhahabu ya alama V shingoni.
Hata hivyo, mama yake mcheza sinema Veronika Loubry, alizitetea picha hizo.
“Kitu pekee kilichonishtusha kuhusu picha ni cheni aliyokuwa ameivaa, ambayo ilikuwa na thamani ya euro milioni tatu (sawa na zaidi Sh bilioni saba za Kitanzania), aliliambia gazeti moja nchini humo.
Picha za jarida hilo lilimkomaza Thylane na kumfanya asirudi nyuma katika dunia ya mitindo.
Sasa akiwa na umri wa miaka 16 amekuwa nembo ya kampuni maarufu ya vipodozi ya L’Oreal Paris tangu Aprili.
Ameshiriki maonesho ya mitindo ya Chanel, Ralph Lauren, Lacoste na hivi karibuni kabisa onesho la kiangazi la Dolce & Gabana.
Kuhusu maisha yake ya sasa, mama yake Loubry anasema ni ya kawaida kama wasichana wengine.
Kwa kuwa mdogo mno, Blondeau hakuweza kupata fursa ya kuzungumza zaidi kuhusu mjadala wa utata aliousababisha bila kujua kipindi kile.
Kadiri alivyokuwa mkubwa, hata hivyo amebakia mwanamitindo maarufu na taratibu ameanza kupaa zaidi kupitia akaunti yake ya Instagram.
Wakati alipokuwa na umri wa miaka 14 alipamba katika vitabu vya IMG Models (wakala wa kimataifa wa mitindo).
“Sehemu niipendayo ya kazi ni kukutana na wapiga picha wapya na wasanii wa urembaji. Napenda kujaribu nguo mpya pia!” aliliambia jarida la Teen Vogue mwaka 2015.
Anachopendelea Blondeau hakijaishia katika dunia ya mitindo pekee bali pia uigizaji kama mama yake. Alionekana katika filamu iitwayo Belle & Sebastian: The Adventure Continues mwaka 2015.
Katika mahojiano mengine, aliulizwa alijisikiaje kuingia katika mitindo katika umri mdogo kiasi kile. Jibu lake lilishangaza lilikuwa la kawaida na hata hakuingia katika mjadala wa utata aliouanzisha
“Sawal, Kate Moss alianza uanamitindo katika umri wa miaka 15, na hilo halikuwa miaka mingi iliyopita. Hivyo, hapana, mimi si mdogo kiasi hicho. Iwapo una wakala mzuri na watu wanaokulinda, hakuna tatizo.”
Oktoba 2016, alihudhuria Wiki ya Mitindo Paris na alifanyiwa mahojiano na Jarida la W, akaulizwa nini atafanya baada ya tukio hilo. Alijibu kwa ufupi jibu la kujitosheleza akionesha namna gani alivyo mkomavu, “kwenda nyumbani kupumzika na kisha kwenda shule.”
Blondeau alitimiza umri wa miaka 16, Aprili 5, 2017. Bado ni mdogo lakini mwenye hekima na busara na kujitambua.
Ana matumaini siku moja atafikia kilele cha mafanikio yake badala ya utata aliousababisha utotoni.