Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MWANDISHI wa habari mwandamizi, Mayage S. Mayage, (56), amefariki dunia jana baada ya kuugua kwa muda.
Mayage alikutwa na umauti katika Hospitali ya Misheni ya Mbweni, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa muda wa wiki mbili.
Taarifa kutoka kwa mdogo wake Emmanuel Mayage, alisema kuwa madaktari waligundua kaka yake kuugua saratani na Kifua Kikuu (TB).
Emmanuel alisema Mayage atazikwa Alhamis Desemba 28, 2017 katika makaburi ya Mbweni, eneo linaloitwa Maputo.
Alisema kwa sasa taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu Mbweni Kijijini, eneo la Maputo ambako ndugu na jamaa wanakutana.
“Mayage aligundulika kuwa na saratani mwaka mmoja uliopita na alianza matibabu katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Ocean Road na Muhimbili,” alisema mdogo huyo wa marehemu.
Alisema hali yake iliimarika kwa muda, lakini ikabadilika wiki tatu zilizopita na kusababisha kulazwa katika Hospitali ya Mbweni.
Emmanuel alisema akiwa hospitalini hapo, kaka yake aligundulika pia kuwa na maradhi ya kifua kikuu na alianzishiwa tiba.
Mayage alianza kazi za uandishi wa habari mwaka 1995, akifanya kazi katika kampuni ya magazeti ya Habari Corporation; inayochapisha magazeti ya MTANZANIA, RAI, Dimba, The African na Bingwa.
Baadaye aliondoka katika magazeti hayo na kuanza kazi ya uandishi wa habari wa kujitegemea, akijiita “mwandishi huru”.
Akiwa mwandishi huru, Mayage alikuwa akiandikia magazeti mbalimbali nchini, yakiwemo ya Raia Tanzania na MwanaHalisi.