AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM
MWANDISHI wa habari wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, ambayo inachapisha magazeti ya MTANZANIA, Rai, Bingwa, Dimba na The African, Eliya Mbonea, amefariki dunia jana wakati akiendelea kutibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Tangu Oktoba mwaka jana, Mbonea alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa nyakati tofauti tofauti.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa familia, Wilfred Hume alisema Mbonea alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kuishiwa damu.
“Wakati huo alianza kuumwa nimonia akapatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC akapona ila baadae akaumwa tena homa ya manjano akafanyiwa operasheni, baada ya hapo miguu ikaanza kuvimba.
“Tukamrudisha tena KCMC wakaja kugundua kuwa alikuwa na uvimbe tumboni, wakamtibu huo uvimbe ikawa hautoki na damu ikawa inamuishia, wakasema tumpeleke Muhimbili,” alisema Hume.
Alisema kuwa Mbonea alivyofika hospitali ya Muhimbili alitibiwa kwa wiki tatu hadi umauti ulipomkuta jana.
“Bado hatujajua atasafirishwa lini kwa sababu kikao hakijakaa ila atazikwa Arusha,” alibainisha Hume.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Claude Gwandu alisema kifo cha Mbonea kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya habari.
“Mbonea pia alikuwa Katibu Mkuu wa APC kuanzia 2010 hadi 2013 na tumekuwa tukishirikiana naye hadi umauti ulipomkuta. Kwetu sisi tumepoteza mtu muhimu sana,” alisema Gwandu.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilitoa salamu za pole kwa uongozi wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited kwa msiba wa Mbonea.
“TEF imeshtushwa na kusikitishwa na taarifa za kifo hicho na hakika kinaacha pengo kubwa siyo tu ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Limited bali kwa tasnia nzima ya habari,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa TEF, Neville Meena.
WASIFU WA MBONEA
Eliya Mbonea alizaliwa Februari 14, 1975 Shinyanga Vijijini, Mkoa wa Shinyanga.
Kuanzia mwaka 1984 hadi 1990 alipata elimu ya msingi Shule ya Msingi Korogwe iliyoko wilayani Kahama mkoani humo.
Kuanzia 1991 hadi 1994 alipata elimu ya kidato cha nne Shule ya Sekondari Kahama iliyoko mkoani Shinyanga.
Agosti, 2002 alihitimu taaluma ya habari ngazi ya cheti katika Chuo cha Tanzania Institute of Media Education (TIME) na kisha kuendelea na chuo hicho mwaka 2002 hadi 2003 alipohitimu masomo katika ngazi ya cheti cha uandishi wa habari.
Mwaka 2007 hadi 2009 alipata mafunzo ya uandishi wa habari katika ngazi ya diploma chuoni hapo.
Kuanzia Januari 2004 hadi 2006 Mbonea alifanya kazi na magazeti ya Majira na Business Times ambayo yanachapishwa na Kampuni ya Business Times Limited (BTL).
Agosti 3, 2006 alijiunga na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd akiandikia gazeti la Rai.
Aidha, Agosti 3, 2010 hadi Mei 31, mwaka jana alikuwa mwakilishi wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd Kanda ya Kaskazini inayojumuhisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.