26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi UDSM aliyejirusha ghorofani asimulia

Pg 1Hadia Khamis na Mwantumu Saadi, Dar es Salaam
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Cecilia Mosha (26) aliyejirusha kutoka ghorofa ya tatu hadi chini kutokana na hofu ya moto uliotokea katika Hosteli ya Mabibo, amevunjika mfupa wa bega.
Mwanafunzi huyo alijirusha kupitia dirishani juzi katika harakati za kujiokoa na moto baada ya jengo la wasichana, Block A kushika moto huku wanafunzi wakiwa vyumbani wakiendelea na shughuli zao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Cecilia ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Uhandisi wa Uchimbaji Madini, alisema alisikia kelele akiwa chumbani na alipotoka nje akakuta moshi umetanda kila kona.
“Baada ya kuona hivyo niliona ni vema nijiokoe kwa kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya bweni hilo hadi chini kupitia dirishani,”alisema Mosha.
Alisema baada ya kuruka hadi chini alikimbizwa katika kituo kidogo cha afya karibu na hosteli hiyo ambako alipoteza fahamu na kushtukia yupo katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).
Naye Meneja Ustawi na Uhusiano wa Taasisi ya MOI, Almasi Jumaa alisema hali ya Cecilia si mbaya na anaendelea na matibabu.
“Tumempokea huyo mgonjwa jana na baada ya timu ya madaktari kumfanyia vipimo vya kutosha wamebaini amevunjika mfupa wa bega la kulia na kupata mshtuko wa mwili … alipata maumivu ya kiuno na mwili kwa ujumla,” alisema Jumaa.
Ajali hiyo ya moto ilitokea juzi katika Hosteli ya Mabibo iliyopo Mtaa wa Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala moto huo uliteketeza ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa na wanafunzi wa kike.
Alisema moto huo haukuwa na madhara kwa binadamu ingawa uliteketeza mali za wanafunzi.
Profesa Mukandali aliahidi uongozi wa chuo utahakikisha wanafunzi hao wanapata msaada wa hali na mali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles