TWALAD SALUM- MWANZA
MWAFUNZI
wa Shule ya Sekondari Koromije wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, amehukumiwa kuchapwa
viboko sita kwa kosa la kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi mwenzake.
Mwendesha Mashitaka mkaguzi msaidizi wa polisi, Juma Kiparo akimsomea hati
ya mashitaka April 2 katika kesi ya jinai namba 8 ya mwaka 2019 mwanafunzi jina
lake limehifadhiwa mwenye umri wa miaka 15 anayesoma kidato cha pili Sekondari
ya Koromije.
Mwendesha mashtaka alimsomea shtaka la kwanza kuwa ni kubaka kinyume cha sheria
kifungu cha 130 (1) 2 (e) na 131 sura 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002, kuwa katika tarehe zisizo fahamika mwaka 2017 na 2018 alifanya mapenzi na
mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 anayesoma shule ya msingi Ibongoya
kinyume cha sheria.
Tuhuma ya Pili kati ya Septemba na Desemba mwaka jana alimpa ujauzito
mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 kinyume cha sheria ya Elimu kifungu cha 60 A
(4) kifungu kidogo cha(4) sura 353 kama ilivyofanyiwa marekebisho ya
sheria 2 mwaka2016.
Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Erick Marley mtuhumiwa alikiri
kufanya kosa hilo na mahakama ikamtia hatiani na kumtaka ajitetee na alisema
kuwa yeye hana wazazi ni mtoto yatima anaishi na bibi na babu yake anaiomba
mahakama impuguzie adhabu.
Mahakama ilimwomba Ofisa Ustawi wa Jamii, Sldvey Mdoe kutoa ushauri.
Katika ushauri wake ofisa huyo aliomba mahakama sheria ifuatwe kulingana na sheria ya mtoto kwani ni kweli mtuhumiwa ni yatima analelewa na bibi na babu yake na mazingira ya malezi ndiyo yamesababisha hali hiyo.
Mahakama ilimuhukumu kosa la kwanza la kubaka apigwe viboko sita, na kosa la pili apigwe viboko sita , badala ya kupigwa viboko 12 atachapwa viboko sita baada ya kupimwa afya yake.