Na Gurian Adolf-NKASI
SERIKALI wilayani Nkasi mkoani Rukwa, imeagiza kukamatwa wazazi wa mwanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Mkinga wilayani hapa ambaye amepata ujauzito, huku wazazi hao wakiwa katika mpango wa kutaka kumuozesha.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, wakati akikabidhi pikipiki 28 zenye thamani ya Sh milioni 98 zilizotolewa na Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mtanda alisema katika Kijiji cha Mkinga kuna mwanafunzi wa darasa la tatu amepata ujauzito na wazazi wake walikua wanaandaa mkakati wa kumuozesha mwanafunzi huyo lakini walishindwa baada ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kuingilia kati na kuvuruga mpango huo.
“Naagiza wazazi wote wa mwanafunzi huyo wakamatwe mara moja, mwanafunzi huyo pamoja na aliyempa mimba mwanafunzi wafikishwe katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake, nanyi waratibu elimu kata tambueni mna jukumu kubwa la kuhakikisha mimba hizi zinakwisha,” alisema Mtanda.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema hali inaonesha bado tatizo la mimba ni kubwa kwani mwezi uliopita jumla ya wanafunzi 27 walipimwa na kubainika kuwa wamepata ujauzito na kueleza kuwa bado kazi kubwa inahitajika katika kupambana na wimbi hilo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Misana Kwangula, alisema lengo la Serikali kuwapatia pikipiki hizo ili waweze kutembelea shule zilizopo katika kata zao kwa kuwa walikuwa wanalalamika kuwa hawana vitendea kazi vya kuwawezesha kufanya ukaguzi katika shule wanazozisimamia.
Mratibu Elimu wa Kata ya Namanyere, Kasilda Milala, aliyekabidhiwa pikipiki kwa niaba ya wenzake aliishukuru Serikali kwani imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya elimu.
Alisema licha ya kutoa vitendea kazi lakini pia inatoa elimu bila malipo hivyo kilichopo ni watendaji wa idara ya elimu pamoja na wanafunzi kuongeza bidii ili kiwango cha ufaulu kiweze kuongezeka wilayani humo.