27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi darasa la tano aozeshwa kwa ng’ombe 8

DAMIAN MASYENENE- SHINYANGA

 WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kumuozesha mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Samuye wilayani Shinyanga umri wa miaka 12 kwa mahari ya ng’ombe 8 na Sh 600,000.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,Debora Magiligimba alisema tukio hilo lilitokea Septemba 14, mwaka huu saa 12:40 jioni Kijiji cha Isela wilayani Shinyanga.

Alisema polisi walibaini kulikuwa na tukio la mtoto mwenye umri wa miaka 12 anafunga ndoa, ndipo kikosi kazi kutoka dawati la jinsia na watoto wakishirikiana na maofisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Shinyanga walifika eneo husika na kukuta sherehe ya harusi ikiendelea nyumbani kwao na bwana harusi.

Kamanda Magiligimba aliwataja waliokamatwa, kuwa ni Geni Bundala (52), Jumanne Shigimahi (54), Hawa Ramadhan (37), na Japhari Khalfan (52) ambao wote ni wakazi wa Kijiji cha Isela.

Alisema wote  walikamatwa wakimuozesha mtoto (jina linahifadhiwa) kwa kijana  Khalfan Japhari (23) mkulima wa kijiji hicho ambaye alitoroka na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

“Uchunguzi wa awali ulibaini  mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 12 aliozeshwa kwa kutolewa mahali ya ng’ombe 8 na fedha tasilimu  shilingi 600,000, mtoto tayari amekabidhiwa kituo cha kulelea watoto ambao ni wahanga wa ukatili na ndoa za utotoni kiitwacho Agape Aids Shinyanga kwa sasa anaendelea na masomo yake,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi  hususani wazazi na walezi mkoani Shinyanga kuacha kuozesha wanafunzi,inapelekea watoto wa kike kukatisha ndoto zao za kuendelea na masomo na hivyo kupelekea kukosa viongozi wanawake wa baadae,  pia wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kutokemeza aina zote ukatili wa kijinsia mkoani shinyanga.

“Naamini kabisa wananchi wakiendelea kuunganisha nguvu ya pamoja na jeshi la polisi dhidi ya uhalifu, tutaweza kuzuia uhalifu, kupunguza uhalifu na kuufanya mkoa wetu wa shinyanga kuendelea kuwa shwari,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles