Walter Mguluchuma-Katavi
JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi, linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Kabungu mwenye umri wa miaka 15 kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi mwenzake wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 17 kwa kumchoma kisu kifuani.
Inaelezwa chanzo cha mauaji hayo, ni ugomvi katia ya wanafunzi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5 usiku Kijiji cha Kagwila wilayani Tanganyika.
Alisema wanafunzi hao walikuwa wakiishi chumba kimoja kutokana na nyumbani kwao kuwa mbali na shule.
Alisema pamoja na mtuhumiwa kusoma kidato cha tofauti na marehemu na kuishi chumba kimoja, katika masuala ya chakula kila mmoja alikuwa anajitegemea kwa kila kitu.
“Siku ya tukio, marehemu alidai alikuwa amenunua mafuta ya kula aina ya Korie mchana ya Sh 300 kwa ajili ya kupikia chakula chake cha usiku.
“Alipotaka kupika hakuyaona mafuta hayo alipokuwa ameyahifadhi ndani ya chumba chao kitendo kilichosababisha kuibuka mzozo,”alisema.
Alisema marehemu alipomuuliza mwenzake kama ametumia mafuta hayo alikana na kwamba hajawahi kuyaona.
Kamanda Nyanda, alisema mzozo ulianza hapo kwa muda mrefu, huku mtuhumiwa akimtuhumu mwenzake kuwa amemwibia na ghafla wakaanza kupigana na mtuhumiwa alizidiwa nguvu na marehemu.
“Mtuhumiwa baada ya kuona amezidiwa nguvu na mwenzake, alichukua kisu na kumchoma nacho kifuani upande wa kushoto, marehemu alipiga yowe akiomba msaada, majirani walifika eneo hilo la tukio. “Walipofungua mlango kwa nguvu walikuta marehemu akigalagala sakafuni huku damu ikiwa imetapakaa,”alisema Kamanda Nyanda .
Alisema majirani walipojaribu kumkimbiza hospitalini kwa matibabu waligundua amekata roho .
“ Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule ya Rufaa Mkoa wa Katavi mjini Mpanda na baada ya kufanyiwa uchunguzi tutawakabidhi ndugu kwa ajili ya mazishi,”alisema.
Hili ni tukio la pili la kutokea kwa vifo vya wanafunzi kwa kipindi cha wiki moja, ambapo hivi karibuni mwanafunzi wa kiume aliyekuwa anasoma darasa la saba Shule ya Msingi Ifukutwa Wilaya ya Tanganyika alijinyonga hadi kufa kutokana na ugumu wa maisha kwa madai wazazi wake walishindwa kumpatia mahitaji ya msingi na kulazimika kufanya vibarua ili ajikimu.