Na FRANCIS GODWIN -IRINGA
JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa, limemsafirisha usiku mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo (24), aliyedai kutekwa na watu wasiojulikana hadi Makao Makuu ya jeshi hilo kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, alimweleza mwandishi wa habari hizi jana kuwa mwanafunzi huyo amesafirishwa usiku na jana asubuhi alikuwa tayari ofisi ya DCI kwa mahojiano juu ya madai yake ya kutekwa.
“Baada ya polisi ngazi ya mkoa kumaliza kazi yetu ya kumhoji na kwa kuwa alisema alitekwa Dar es Salaam tulilazimika kumsafirisha hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa na DCI pamoja na kuonyesha eneo ambalo walimteka.”
Kamanda Bwire alisema kwa sasa wanamwomba mtu aliyejitambulisha kwenye mitandao kwa jina la Jonathan Kwepe, ili kulisaidia Jeshi la Polisi kujua ukweli zaidi wa tukio hilo kwa kuwa inaonyesha alisafiri naye na walikaa siti moja.
Pamoja na kumwomba Kwepe kujitokeza pia alitoa rai kwa wananchi wengine wenye taarifa zaidi za Nondo, kujitokeza ili kusaidia kupata ukweli wa jambo hilo.
Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP), alidai kutekwa na watu wasiojulikana kabla ya Machi 7, mwaka huu na taarifa zake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii kabla ya jioni kuripotiwa kupatikana akiwa hajitambui na kwenda kituo cha polisi Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kuripoti kutekwa kwake.
Hata hivyo, taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa iliyotolewa Machi 8 saa 4.45 na Kamanda wa Polisi Mkoa, ilidai kuwa Nondo alipatikana Machi 7, mwaka huu saa 1 asubuhi baada ya kufika Kituo kidogo cha polisi Mafinga Wilaya ya Mufindi na kueleza kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.
Tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama alikuwa ametekwa na kama kweli wahusika watasakwa na kama si kweli sheria itachukuwa mkondo wake dhidi ya Nondo.
Taarifa za kutekwa kwa Nondo ziliwalazimu wanafunzi wenzake kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kupewa RB namba; UD/RB/1438/2018.
Kwa mujibu wa wanafunzi wenzake kabla ya Nondo kudaiwa kutekwa aliandika ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani uliosomeka ‘Iam at High Risk’ akiwa na maana yuko hatarini na baada ya hapo hakupatikana tena hadi alipoonekana Mafinga.
Mwandishi wa habari hizi jana alifika katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga kutaka kujua kama Nondo alipatiwa matibabu ambapo Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Innocent Mhagama, alisema jina la mwanafunzi huyo halimo kwenye kumbukumbu ya wagonjwa waliofika hospitalini hapo.
MTANZANIA Jumamosi jana liliwasiliana na DCI, Robert Boaz, kwa njia ya simu ili kufahamu kama amempokea Nondo ambapo aliomba atafutwe kwa njia ya ujumbe mfupi kwani muda huo saa 11 jioni alikuwa kwenye kikao.
Alipotumiwa ujumbe mfupi, DCI Boaz hakujibu, gazeti hili linaendelea kufuatilia tukio hili.