Na Amina Omari -Muheza
MGOMBEA ubunge Jimbo la Muheza, Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA (CCM), amesema atahakikisha yeye ni kitabu kipya chenye mawazo tofauti na yupo tayari kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za jimbo hilo zilizoshirikisha viongozi mbalimbali na wasanii kama sehemu ya kumuunga mkono.
MwanaFA alisema atahakikisha anazisema changamoto za wana-Muheza bungeni na kuwaomba wananchi kutoa kura za kutosha kwa chama chake.
Alisema atahakikisha anawatua kina mama ndoo kichwani kwa kuwasogezea huduma za maji karibu yao kwa kuendeleza mradi wa maji ulioanzishwa na mbunge aliyepita, Balozi Adadi Rajab.
”Matatizo ya Muheza hayana rangi kama yataacha kuona kuna sehemu, nataka kupambana nayo, nipeni madiwani wote 37 tukawatumikie wananchi, tunataka kuhakikisha tunakuwa na Muheza mpya yenye maendeleo,” alisema MwanaFA ambaye ni msanii wa muziki wa kizazi kipya.
Kuhusu barabara, alisema atalala kwa waziri na katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya kuhakikisha barabara ya Amani inatengenezwa kwa kiwango cha lami.
”Nitakwenda kulala kwa waziri wa ujenzi mpaka kieleweke, lengo ni kuhakikisha tunakuwa na Muheza mpya yenye maendeleo. Chama kilinichagua kikijua kinachagua mtu mbishi wa kushughulikia changamoto,” alisema MwanaFA.
Alisema atashughulikia changamoto ya afya kwa kuhakikisha vinakuwepo vituo vya afya vya kutosha katika kila kata, huku upande wa elimu akiahidi kuwepo kwa shule zinazotoa elimu ya juu katika maeneo mengi.
Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Balozi Adadi, aliwataka wananchi kuondoa makundi ya ‘team Adadi’ na ‘team MwanaFA’, badala yake wahakikishe wanaipatia Muheza ushindi wa kishindo.
Alisema atahakikisha anampa ushirikiano wa kutosha ili mwisho wa siku waibuke na ushindi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu aliwataka wakazi wa mkoa huo kuacha kuyumbishwa na vyama vingine na kuwataka kusimama imara kwa maendeleo ya nchi kwani mambo mengi muhimu yamefanyika nchini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema wana-Muheza wana bahati kupata kijana mahiri na mnyenyekevu ili ayaendeleze yale aliyoyafanya balozi Adadi.