Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’, leo Februari 7, 2024 amezinduzi ofisi za Klabu ya Yanga zilizopo Jangwani jijini Dar es Salaam baada ya kufanyiwa maboresho.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwana FA ameupongeza uongozi wa Yanga kwa kitu walichofanya kwani kutokana na jengo hilo ni la zamani ilikuwa siyo rahisi kuamini kama kuna shughuli za ukarabati zingefanyika.
“Nimekuwa nikipita hapa Jangwani sijawahi kufahamu kama kuna shughuli zinaendelea humu ndani. Lakini kwa hili ambalo mmelifanya, kweli ni ishara thabiti ya namna klabu kubwa inavyofanya mambo yake. Nilidhani Injinia Hersi Said (Rais wa Klabu ya Yanga) umekata tamaa lakini kumbe ulikuwa na mpango mkubwa,” amesema Mwana FA.
Amesema uboreshaji huo wa jengo hilo, ni maendeleo ambayo klabu kubwa kama Yanga inatakiwa kufanya.
Ameeleza kuwa uwepo wa jengo hilo lililojengwa miaka 53 ni maono ya wazee wa zamani akiwamo, Hayati Abeid Amani Karume ambaye alifikiria na kuweka nguvu zake na hadi leo jengo linaweza kuhudumia klabu ya mwaka 2024.
Kwa upande wake Rais wa Yanga, Injinia Hersi ameweka wazi kuwa ofisi hizo zimefanyiwa ukarabati kwa miaka mitatu.