Na Ras Inno,
JUMA moja lililopita Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Duniani ‘Amnesty International’ lilitoa taarifa iliyotonesha kidonda cha madhila yaliyotokea nchini Nigeria miongo mitatu na nusu na ushei iliyopita, ambayo inawezekana dunia imeshayasau kutokana na kuangazia zaidi migogoro mingine inayofukuta kwa sasa katika maeneo mbalimbali.
Serikali ya Nigeria imekanusha vikali yaliyobainishwa katika taarifa hiyo ya Amnesty inayotaja matukio ya mwaka mmoja uliopita lakini ikikumbusha machungu ambayo bado hayajasahaulika kwa walioumizwa.
Ripoti hiyo imebainisha kwamba vikosi vya usalama vya Serikali vimewaua watu takribani 150 katika maandamano ya kuunga mkono jimbo lililoko Kusini Mashariki la Biafra linalotaka kujitenga, kwa kuwatwanga risasi waandamanaji wanachama wa kundi la waasilia wa Biafra (IPOB) katika matukio mbalimbali kwa muda wa mwaka mmoja uliopita hadi Agosti mwaka huu.
Ni vuguvugu jipya linalozidi kukanganya mustakabali wa utulivu wa Taifa hilo kubwa barani Afrika, kwa kuwa bado halijamaliza matatizo ya Boko Haram Kaskazini Mashariki na sekeseke linaloendelea katika jimbo la Kusini la Delta. Kilichoanzisha hamkani mpya Biafra ni mwendelezo wa manung’uniko ya watu wa kabila la Igbo wanaoishi huko kwa eneo lao kupuuzwa kwa ukosefu wa maendeleo, miundombinu duni ya huduma za kijamii zikiwamo hospitali na shule pia wanasiasa weledi kutoka eneo hilo kutoteuliwa kushika nyadhifa serikalini.
Vuguvugu hilo jipya liliibuka baada ya kiongozi wa IPOB, Nnamndi Kanu kutiwa kizuizini aliporejea Nigeria kutoka Uingereza anakoishi na kufunguliwa mashtaka ya uhaini kutokana na kuendesha redio yake jijini London inayodaiwa kuchochea kushambuliwa kwa vikosi vya Serikali.
Kinachobainishwa na Amnesty ni kikonyo tu cha kina halisi kilichotokea wakati wa vita ya Biafra iliyorindima kuanzia mwaka 1967 hadi 1970, wakati jimbo hilo lililipojitangazia madaraka kamili na kujipa jina kutokana na ghuba iliyoko Kusini mwake na kujumuisha makabila mengine ya Waefik, Waibibio, Waanang, Waejang, Waeket, Waibeno na Waijaw.
Taifa hilo lililojitenga lilisababisha mgawanyiko wa msimamo kwa wanachama wa umoja wa nchi huru za Afrika kwa kutambuliwa rasmi na nchi za Gabon, Tanzania, Ivory Coast na Zambia na nje ya Afrika lilitambuliwa na visiwa vya Haiti na kupata msaada kutoka kwa baadhi ya nchi zikiwamo Israel, Ufaransa, Uhispania na jumuya mbalimbali za kidini. Lakini baada ya mapigano ya miaka miwili na nusu Biafra ilishindwa na kurudishwa upya kwa Nigeria, kutokana na mbinu iliyolaaniwa vikali duniani kote iliyotumiwa na majeshi ya Nigeria kwamba “adui yako msababishie njaa” kwa kulizingira jimbo hilo na kusababisha baa la njaa lililoua wakazi milioni tatu wa eneo hilo.
Kimsingi Biafra ilidaiwa kuwapo kabla hata Nigeria haijapata uhuru kutoka kwa wakoloni, kwa jina la ‘Biafara’ ikiunganisha maneno ghuba ‘Bay’ iliyokaliwa na watu wanaotokana na kizazi cha ‘Ephraim’ kwa kujinasibisha na Mto Nun ulioko Kusini mwa Nigeria ambalo ni jina la baba wa Joshua wa kabila la Ephraim anayesimuliwa kwenye Biblia linalomaanisha: ‘Baraka ya Mungu’ kwenye nchi aliyopewa.
Kwa kuamini hivyo ubishani uliozaa mkanganyiko huo unasababishwa na mgawanyiko wa kiimani unaoligubika Taifa la Nigeria, ingawa kinachoigusa dunia kutokana na ripoti ya Amnesty hakihusiani na mashiko hayo bali haki za binadamu zinazokandamizwa, hususani ikikumbukwa kuwa Rais wa sasa wa Nigeria Muhammadu Buhari aliyewahi kutawala kijeshi mnamo miaka ya 1980 alikuwa Brigedia Meja aliyeongoza vikosi vya Serikali dhidi ya majeshi ya Biafra katika mapambano hayo, ambapo majeshi hayo yalishutumiwa kwa ukatili mkubwa na ni Buhari huyo huyo aliyetamka mwaka jana kuwa kulikoni kuruhusu vuguvugu la harakati za Biafra kujitenga kuibuka upya na kuligawanya Taifa la Nigeria, ni heri Taifa zima lizame bahari na kuangamia.
Ni msimamo unaodhihirisha kuwa mgogoro huo haujamalizika bado kwani mashiko yaliyogawa msimamo wa OAU bado yanazua hisia, hata wakati Mwalimu Nyerere alipotetea msimamo wa Taifa letu kuitambua Biafra alisisitiza kuwa: “Kutokana na imani kwamba kila binadamu duniani anastahili kuwa na mahala anapopaita kwake bila kubughudhiwa, lakini wanachofanyiwa sasa watu wa Biafra ni sawa na Wayahudi walivyofanyiwa na Hitler ingawa wamebahatika kupata nchi waliyokimbilia kujinusuru na kujitangazia uhuru.
Kwa muktadha huo tunalazimika kukosoa mgawanyiko wa OAU na kuitambua Biafra kama Taifa kamili ili kutimiza dhima kuwa madhumuni ya jamii na mifumo ya kisiasa ni kuwastawisha wanadamu”.
Biafra ni kama pembe la ng’ombe lisilofichika lililoibuliwa upya kwa taarifa ya Amesty International na kukumbusha vuguvugu la mgawanyiko uliojitokeza wakati wa vita ya kujitenga, ingawa nchi nyingi barani Afrika ziliiunga mkono Serikali ya Nigeria iliyoongozwa na Jenerali Yakubu Gowon dhidi ya vikosi vya Biafra vilivyoongozwa na Chukwuemeka Odumegwu Ojukwu lakini zilifanya hivyo kwa kuhofia kufanikiwa kujitenga kwa Biafra kungeamsha hamasa za jamii zilizotaka kujitenga ndani ya mataifa mengine barani hapa.
Ingawaje Afrika haijawahi kufanikiwa kuwa na sauti moja dhidi ya migogoro mingi huku mingine ikisababisha mapigano yanayoishia kufanikiwa kujitenga na kuanzishwa taifa jipya, kama ilivyotokea kwa Eritrea iliyopigana na kujitenga kutoka Ethiopia.