Ramadhan Hassan -Dodoma
WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Dk.Harrison Mwakyembe amesema anashangaa ni kwa nini makocha wa kigeni wanakuja kufanya kazi nchini wakiwa na wasaidizi wao hivyo ameshauri makocha wasaidizi wawe wazawa.
Akihitimisha hoja zilizojadiliwa na wabunge, Mwakyembe alisema:
“Wasaidizi watafutiwe hapa hapa nchini kocha kutoka nje anakuja na wasaidizi ni kuongeza gharama tu hasa kwenye hizi klabu zetu, hili liangalieni sana,”alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe alisema kwa sasa kuna wasanii 1934, ambapo Serikali inafuatilia ili kujua kila msanii anatakiwa kulipwa kiasi gani kutokana na kazi zake.
“Kwa sasa tuna orodha ya wasanii 1934 na tunafuatilia ni kiasi gani cha fedha wanatakiwa kulipwa, hata waheshimiwa wabunge ambao ni wasanii pia tunawaona, namuona namba 886 ni Martha Mlata, Namuona Profesa J namba 1351,”alisema.
Kuhusu kuongeza bajeti ya Taasisi ya Bagamoyo (Tasuba) alisema, imeombewa Shmilioni 250.
“Naamini bunge lako litapitisha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na vifaa vya kufundishia,”alisema.
Kuhusiana na kushirikishwa sekta binafsi katika kujenga miundombinu,Waziri Mwakyembe alisema wameanza ujenzi wa kituo cha michezo na watashirkisha sekta binafsi.